55

Sala ya mtu anayedhulumiwa
(Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Utenzi wa Daudi)
1 Ee Mungu, tega sikio usikie sala yangu; usiangalie pembeni ninapokuomba.
2 Unisikilize na kunijibu; nimechoshwa na lalamiko langu.
3 Nina hofu kwa vitisho vya maadui zangu, na kwa kudhulumiwa na watu waovu. Watu waovu wananitaabisha, kwa hasira wananifanyia uhasama.
4 Moyo wangu umejaa hofu, vitisho vya kifo vimenisonga.
5 Natetemeka kwa hofu kubwa, nimevamiwa na vitisho vikubwa.
6 Laiti ningekuwa na mabawa kama njiwa! Ningeruka mbali na kupata pumziko;
7 naam, ningesafiri mbali sana, na kupata makao jangwani.
8 Ningekimbilia mahali pa usalama, mbali na upepo mkali na dhoruba.
9 Ee Bwana, uwaangamize na kuvuruga lugha yao; maana naona ukatili na ugomvi mjini,
10 vikiuzunguka usiku na mchana, na kuujaza maafa na jinai.
11 Uharibifu umeenea pote mjini, uhasama na udhalimu kila mahali.
12 Kama adui yangu angenitukana, ningeweza kustahimili hayo; kama mpinzani wangu angenidharau, ningeweza kujificha mbali naye.
13 Kumbe, lakini, ni wewe mwenzangu; ni wewe rafiki yangu na msiri wangu!
14 Sisi tulizoea kuzungumza kirafiki; pamoja tulikwenda nyumbani kwa Mungu.
15 Acha kifo kiwafumanie maadui zangu; washuke chini Kuzimu wangali hai; maana uovu umewajaa moyoni mwao.
16 Lakini mimi namlilia Mungu, naye Mwenyezi-Mungu ataniokoa.
17 Jioni, asubuhi na adhuhuri, nalalama na kulia, naye ataisikia sauti yangu.
18 Atanikomboa salama katika vita ninayoikabili, kwa maana maadui zangu ni wengi.
19 Mungu atawalaye tangu milele, atanisikia na kuwaaibisha maadui zangu, maana hawapendi kujirekebisha, wala hawamwogopi Mungu.
20 Mwenzangu amewashambulia rafiki yake, amevunja mapatano yake.
21 Maneno yake ni laini kuliko siagi, lakini mawazo yake ni ya kufanya vita. Maneno yake ni mororo kama mafuta, lakini yanakata kama upanga mkali.
22 Mwachie Mwenyezi-Mungu mzigo wako, naye atakutegemeza; kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe.
23 Wewe, ee Mungu, utawaporomosha shimoni chini kabisa, watu hao wauaji na wadanganyifu; hao hawatafikia nusu ya maisha yao. Lakini mimi nitakutumainia wewe ee Mungu!

Generic placeholder image