KITABU CHA PILI(Zaburi 42–72) 42
Sala ya Mkimbizi(Kwa Mwimbishaji. Utenzi wa Wakorahi) 1 Kama paa atamanivyo maji ya kijito, ndivyo ninavyokutamani, ee Mungu wangu! 2 Naona kiu ya Mungu, kiu ya Mungu aliye hai. Nitafika lini kwake na kuuona uso wake? 3 Machozi yamekuwa chakula changu mchana na usiku, waliponiambia kila siku: “Yuko wapi Mungu Wako!” 4 Nakumbuka tena mambo haya kwa majonzi moyoni mwangu: Jinsi nilivyokwenda na umati wa watu, nikawaongoza kwenda nyumbani kwa Mungu wakipiga vigelegele vya shukrani; umati wa watu wakifanya sherehe! 5 Mbona nasononeka hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo ndani mwangu? Nitamtumainia Mungu, maana nitamsifu tena yeye aliye msaada wangu na Mungu wangu. 6 Nimesongwa na huzuni moyoni mwangu, kwa hiyo ninakukumbuka wewe, ee Mungu, kutoka katika eneo la Yordani, kutoka mlima Hermoni na Mizari. 7 Nimeporomoshewa mafuriko ya maji mafuriko ya maji yaja karibu nayo yaita maporomoko mapya. Mawimbi na mapigo yako yamenikumba. 8 Mwenyezi-Mungu atanijalia fadhili zake mchana; nami nimwimbie wimbo wa sifa usiku, nimwombe Mungu anipaye uhai. 9 Namwambia Mungu, mwamba wangu: “Kwa nini umenisahau? Yanini niende huko na huko nikiomboleza kwa kudhulumiwa na adui yangu?” 10 Nimepondwa kwa matukano yao, wanaponiuliza kila siku: “Yuko wapi, Mungu wako!” 11 Mbona nasononeka hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo? Nitamtumainia Mungu, maana nitamsifu tena Mungu, aliye msaada wangu na Mungu wangu.