119

Sheria ya Mungu
1 Heri watu wanaoishi bila kosa, wanaozingatia sheria ya Mwenyezi-Mungu.
2 Heri wanaozingatia matakwa yake, wanaomtafuta kwa moyo wao wote,
3 watu wasiotenda uovu kamwe, bali daima hufuata njia zake.
4 Ee Mungu, umetupatia kanuni zako ili tuzishike kwa uaminifu.
5 Laiti mwenendo wangu ungeimarika, kwa kuyafuata masharti yako!
6 Nikizingatia amri zako zote, hapo kweli sitaaibishwa.
7 Nitakusifu kwa moyo mnyofu, nikijifunza maagizo yako maadilifu.
8 Nitayafuata masharti yako; usiniache hata kidogo.

Kutii sheria ya Mungu
9 Kijana atatunzaje maisha yake kuwa safi? Kwa kuyaongoza kadiri ya neno lako.
10 Najitahidi kukutii kwa moyo wote; usiniache nikiuke amri zako.
11 Nimeshika neno lako moyoni mwangu, nisije nikakukosea.
12 Utukuzwe, ee Mwenyezi-Mungu! Unifundishe masharti yako.
13 Nitayarudia kwa sauti maagizo yako yote uliyotoa.
14 Nafurahi kufuata maamuzi yako, kuliko kuwa na utajiri mwingi.
15 Nazitafakari kanuni zako, na kuzizingatia njia zako.
16 Nayafurahia masharti yako; sitalisahau neno lako.

Kufurahia sheria ya Mungu
17 Unitendee mimi mtumishi wako kwa ukarimu, nipate kuishi na kushika neno lako.
18 Uyafumbue macho yangu, niyaone maajabu ya sheria yako.
19 Mimi ni mkimbizi tu hapa duniani; usinifiche amri zako.
20 Roho yangu yaugua kwa hamu kubwa ya kutaka kujua daima maagizo yako.
21 Wewe wawakemea wenye kiburi, walaanifu, ambao wanakiuka amri zako.
22 Uniepushe na matusi na madharau yao, maana nimeyazingatia maamuzi yako.
23 Hata kama wakuu wanakula njama dhidi yangu; mimi mtumishi wako nitayatafakari maamuzi yako.
24 Masharti yako ni furaha yangu; hayo ni washauri wangu.

Kushika sheria ya Mungu
25 Nagaagaa chini mavumbini; unipe tena uhai kama ulivyoahidi.
26 Nimeungama niliyotenda, nawe ukanijibu; unifundishe masharti yako.
27 Unifundishe namna ya kushika kanuni zako, nami nitayatafakari matendo yako ya ajabu.
28 Niko hoi kwa uchungu; unirudishie nguvu kama ulivyoahidi.
29 Uniepushe na njia za upotovu; unifundishe kwa wema sheria yako.
30 Nimechagua njia ya uaminifu; nimezingatia maagizo yako.
31 Nazingatia maamuzi yako, ee Mwenyezi-Mungu; usikubali niaibishwe!
32 Nitafuata maelekezo ya amri zako, maana unanipa maarifa zaidi.

Kuomba maarifa
33 Ee Mwenyezi-Mungu, unifundishe kutii masharti yako; nami nitayashika mpaka mwisho.
34 Unieleweshe nipate kuishika sheria yako, niifuate kwa moyo wangu wote.
35 Uniongoze katika njia ya amri zako, maana humo napata furaha yangu.
36 Unipe ari ya kuzingatia maamuzi yako, na si kwa ajili ya kupata faida isiyofaa.
37 Uniepushe, nisifuate mambo ya upuuzi; unioneshe njia yako, unipe uhai.
38 Unitimizie mimi mtumishi wako ahadi yako; ahadi unayowapa wale wanaokuheshimu.
39 Uniokoe na lawama ninazoogopa; maana maagizo yako ni mema.
40 Natamani sana kuzitii kanuni zako; unijalie uhai maana wewe ni mwadilifu.

Kutegemea sheria ya Mungu
41 Fadhili zako zinijie, ee Mwenyezi-Mungu; uniokoe kama ulivyoahidi.
42 Hapo nitaweza kuwajibu hao wanaonitukana, maana mimi nina imani sana na neno lako.
43 Unijalie kusema ukweli wako daima, maana tumaini langu liko katika maagizo yako.
44 Nitatii sheria yako daima, nitaishika milele na milele.
45 Nitaishi katika uhuru kamili, maana nazitilia maanani kanuni zako.
46 Nitawatangazia wafalme maamuzi yako, wala sitaona aibu.
47 Furaha yangu ni kuzitii amri zako, ambazo mimi nazipenda.
48 Naziheshimu na kuzipenda amri zako; nitayatafakari masharti yako.

Kuwa na imani na sheria ya Mungu
49 Ukumbuke ahadi yako kwangu mimi mtumishi wako, ahadi ambayo imenipa matumaini.
50 Hata niwapo taabuni napata kitulizo, maana ahadi yako yanipa uhai.
51 Wasiomjali Mungu hunidharau daima, lakini mimi sikiuki sheria yako.
52 Ninapoyakumbuka maagizo yako ya tangu kale, nafarijika, ee Mwenyezi-Mungu.
53 Nashikwa na hasira kali, nionapo waovu wakivunja sheria yako.
54 Masharti yako yamekuwa wimbo wangu, nikiwa huku ugenini.
55 Usiku ninakukumbuka, ee Mwenyezi-Mungu, na kushika sheria yako.
56 Hii ni baraka kubwa kwangu, kwamba nazishika kanuni zako.

Heshima kwa sheria ya Mungu
57 Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ndiwe riziki yangu kuu; naahidi kushika maneno yako.
58 Naomba radhi yako kwa moyo wangu wote; unionee huruma kama ulivyoahidi!
59 Nimeufikiria mwenendo wangu, na nimerudi nifuate maamuzi yako.
60 Bila kukawia nafanya haraka kuzishika amri zako.
61 Waovu wametega mitego waninase, lakini mimi sisahau sheria yako.
62 Usiku wa manane naamka kukusifu, kwa sababu ya maagizo yako maadilifu.
63 Mimi ni rafiki ya wote wakuchao, rafiki yao wanaozitii kanuni zako.
64 Dunia imejaa fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, unifundishe masharti yako.

Ukamilifu wa sheria ya Mungu
65 Umenitendea vema mimi mtumishi wako, kama ulivyoahidi, ee Mwenyezi-Mungu.
66 Unifundishe akili na maarifa, maana nina imani sana na amri zako.
67 Kabla ya kuniadhibu nilikuwa nikikosea, lakini sasa nashika neno lako.
68 Wewe ni mwema na mfadhili; unifundishe masharti yako.
69 Wenye kiburi wanasema uongo juu yangu, lakini mimi nashika kanuni zako kwa moyo wote.
70 Mioyo yao imejaa upumbavu, lakini mimi nafurahia sheria yako.
71 Nimefaidika kutokana na taabu yangu, maana imenifanya nijifunze masharti yako.
72 Sheria uliyoweka ni bora kwangu, kuliko mali zote za dunia.

Ukamilifu wa sheria ya Mungu
73 Mikono yako iliniumba na kuniunda; unijalie akili nijifunze amri zako.
74 Wakuchao wataniona na kufurahi, maana tumaini langu liko katika neno lako.
75 Najua hukumu zako ni adili, ee Mwenyezi-Mungu, na kwamba umeniadhibu kwani wewe ni mwaminifu.
76 Fadhili zako na zinipe faraja, kama ulivyoniahidi mimi mtumishi wako.
77 Unionee huruma nipate kuishi, maana sheria yako ni furaha yangu.
78 Wenye kiburi waaibike kwa maana wamenifanyia hila, lakini mimi nitazitafakari kanuni zako.
79 Wote wakuchao na waje kwangu, wapate kuyajua maamuzi yako.
80 Moyo wangu na uzingatie masharti yako, nisije nikaaibishwa.

Sala wakati wa kudhulumiwa
81 Niko hoi kwa kukungojea uniokoe; naweka tumaini langu katika neno lako.
82 Macho yangu yanafifia nikingojea ulichoahidi. Nauliza: “Utakuja lini kunifariji?”
83 Nimekunjamana kama kiriba katika moshi, hata hivyo sijasahau masharti yako.
84 Mimi mtumishi wako nitasubiri mpaka lini? Utawaadhibu lini wale wanaonidhulumu?
85 Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, watu ambao hawafuati sheria yako.
86 Amri zako zote ni za kuaminika; watu wananitesa bila haki; unisaidie!
87 Karibu wangefaulu kuniangamiza, lakini mimi sijavunja kanuni zako.
88 Unisalimishe kadiri ya fadhili zako, nipate kuzingatia maamuzi uliyotamka.

Sheria ya Mungu ni ya kutegemewa
89 Neno lako, ee Mwenyezi-Mungu, ladumu milele; limethibitika juu mbinguni.
90 Uaminifu wako wadumu vizazi vyote, umeiweka dunia mahali pake nayo yadumu.
91 Kwa amri yako viumbe vyote vipo leo, maana vitu vyote ni watumishi wako.
92 Kama sheria yako isingekuwa furaha yangu, ningalikwisha angamia kwa taabu zangu.
93 Sitasahau kamwe kanuni zako, maana kwa hizo umenipa uhai.
94 Mimi ni wako, uniokoe, maana nimejitahidi kuzishika kanuni zako.
95 Waovu wanivizia wapate kuniua; lakini mimi natafakari masharti yako.
96 Nimetambua kila kitu hufikia kikomo, lakini amri yako ni kamilifu.

Kuipenda sheria ya Mungu
97 Naipenda sana sheria yako! Naitafakari mchana kutwa!
98 Amri yako iko nami daima, yanipa hekima kuliko maadui zangu.
99 Ninaelewa kuliko waalimu wangu wote, kwa kuwa nayatafakari maamuzi yako.
100 Nawapita wazee kwa busara yangu, kwa sababu nazishika kanuni zako.
101 Najizuia nisifuate njia mbaya, nipate kulizingatia neno lako.
102 Sikukiuka maagizo yako, maana wewe mwenyewe ulinifundisha.
103 Maneno yako ni matamu sana kwangu; naam, ni matamu kuliko asali!
104 Kwa kanuni zako napata hekima, kwa hiyo nachukia kila mwenendo mbaya.

Sheria ya Mungu ni mwanga
105 Neno lako ni taa ya kuniongoza, na mwanga katika njia yangu.
106 Nimeapa na kuthibitisha kiapo changu, kwamba nitashika maagizo yako adili.
107 Ee Mwenyezi-Mungu, ninateseka mno; unijalie uhai kama ulivyoahidi.
108 Ee Mwenyezi-Mungu, upokee sala yangu ya shukrani; na kunifundisha maagizo yako.
109 Maisha yangu yamo hatarini daima, lakini siisahau sheria yako.
110 Waovu wamenitegea mitego, lakini sikiuki kanuni zako.
111 Maamuzi yako ni riziki kubwa kwangu milele; hayo ni furaha ya moyo wangu.
112 Nimekusudia kwa moyo wote kufuata masharti yako milele.

Usalama katika sheria ya Mungu
113 Nawachukia watu wanafiki, lakini naipenda sheria yako.
114 Wewe ni ngao yangu, kwako napata usalama; aweka tumaini langu katika neno lako.
115 Ondokeni kwangu, enyi waovu, ili nipate kushika amri za Mungu wangu.
116 Uniimarishe ulivyoahidi, nami nitaishi; usikubali niaibike katika tumaini langu.
117 Unitegemeze, niwe salama; niwe daima msikivu kwa masharti yako.
118 Unawakataa wote wanaokiuka masharti yako; mawazo yao maovu ni ya bure.
119 Waovu wote wawaona kuwa takataka, kwa hiyo mimi napenda maamuzi yako.
120 Natetemeka kwa kukuogopa wewe; nimejaa hofu kwa sababu ya hukumu zako.

Utii wa sheria ya Mungu
121 Nimefanya mambo mema na adili; usiniache makuchani mwa maadui zangu.
122 Uahidi kunisaidia mimi mtumishi wako; usikubali wenye kiburi wanidhulumu.
123 Macho yangu yanafifia nikingojea uniokoe, nikingojea utimize uliyoahidi.
124 Unitendee mimi mtumishi wako kadiri ya wema wako, unifundishe masharti yako.
125 Mimi ni mtumishi wako, unipe maarifa, nipate kujua maamuzi yako.
126 Ee Mwenyezi-Mungu, sasa ni wakati wa kufanya kitu, kwa maana watu wanavunja sheria yako.
127 Mimi, nazipenda amri zako, kuliko hata dhahabu safi kabisa.
128 Kwa hiyo, nafuata kanuni zako zote; kila njia potovu naichukia.

Hamu ya kutii sheria za Mungu
129 Maamuzi yako ni ya ajabu; kwa hiyo nayashika kwa moyo wote.
130 Maelezo ya mafundisho yako huleta mwanga; huwapa akili watu wasiojua kitu.
131 Nafungua kinywa kwa hamu kubwa, maana ninatamani sana amri zako.
132 Unigeukie na kunionea huruma, kama uwatendeavyo wanaokupenda.
133 Uniimarishie hatua zangu kama ulivyoahidi; usikubali mimi nitawaliwe na uovu.
134 Unikomboe kutoka udhalimu wa binadamu, ili nipate kuzishika kanuni zako.
135 Uniangazie uso wako kwa wema, unifundishe masharti yako.
136 Macho yangu yabubujika machozi kama mto, kwa sababu watu hawaishiki sheria yako.

Ukamilifu wa sheria ya Mungu
137 Ee Mwenyezi-Mungu, wewe ni mwadilifu; na hukumu zako ni za haki.
138 Umetoa maamuzi yako, kwa haki na uthabiti.
139 Upendo wangu kwako wanifanya niwake hasira, maana maadui zangu hawajali maneno yako.
140 Ahadi yako ni hakika kabisa, nami mtumishi wako naipenda.
141 Mimi ni mdogo na ninadharauliwa; hata hivyo sisahau kanuni zako.
142 Uadilifu wako ni wa haki milele; sheria yako ni ya kweli.
143 Taabu na huzuni vimenipata, lakini amri zako ndizo furaha yangu.
144 Maamuzi yako ni ya haki daima; unijalie maarifa nipate kuishi.

Kuomba usalama
145 Nakulilia kwa moyo wangu wote; unijibu, ee Mwenyezi-Mungu, nifuate kanuni zako.
146 Nakulilia, unisalimishe; nipate kuyazingatia maamuzi yako.
147 Naamka kabla ya pambazuko na kukuomba msaada; naweka tumaini langu katika maneno yako.
148 Nakaa macho usiku kucha, ili nitafakari juu ya maagizo yako.
149 Kwa fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, unisikie; unisalimishe kwa uadilifu wako.
150 Wale wanaonidhulumu vibaya wanakaribia, hao wako mbali kabisa na sheria yako.
151 Lakini wewe u karibu nami, ee Mwenyezi-Mungu, na amri zako zote ni za kuaminika.
152 Tangu zamani, nimejifunza maamuzi yako; ambayo umeyaweka hata yadumu milele.

Kuomba msaada
153 Uangalie mateso yangu, uniokoe, kwa maana sikuisahau sheria yako.
154 Unitetee na kunikomboa; unijalie uhai kama ulivyoahidi.
155 Waovu hawataokolewa kamwe, maana hawajali juu ya masharti yako.
156 Huruma yako ni kubwa, ee Mwenyezi-Mungu, unijalie uhai kama ulivyoahidi.
157 Maadui na wadhalimu wangu ni wengi, lakini mimi sikiuki maamuzi yako.
158 Niwaonapo wahaini hao nachukizwa mno, kwa sababu hawazishiki amri zako.
159 Tazama, ee Mungu, ninavyozipenda kanuni zako! Unijalie uhai kadiri ya fadhili zako.
160 Kitovu cha neno lako ni ukweli, maagizo yako yote adili, yadumu milele.

Kuzingatia sheria ya Mungu
161 Wakuu wanidhulumu bila kisa, lakini mimi naheshimu maneno yako kwa moyo wote.
162 Nafurahi kwa sababu ya neno lako, kama mtu aliyekuta kitu cha thamani kuu.
163 Nachukia kabisa uongo, lakini naipenda sheria yako.
164 Nakusifu mara saba kila siku, kwa sababu ya maagizo yako adili.
165 Wapendao sheria yako wana amani kuu; hakuna kinachoweza kuwaangusha.
166 Ee Mwenyezi-Mungu, nakungojea uniokoe; mimi natimiza amri zako.
167 Nazingatia maamuzi yako; nayapenda kwa moyo wote.
168 Nazingatia kanuni na maamuzi yako; wewe wauona mwenendo wangu wote.

Kuomba msaada
169 Kilio changu kikufikie, ee Mwenyezi-Mungu! Unijalie akili kama ulivyoahidi.
170 Ombi langu likufikie; uniokoe kama ulivyoahidi.
171 Nitasema sifa zako mfululizo, maana wanifundisha masharti yako.
172 Nitaimba juu ya neno lako, maana amri zako zote ni za haki.
173 Uwe daima tayari kunisaidia, maana nimeamua kufuata kanuni zako.
174 Natazamia sana uniokoe, ee Mwenyezi-Mungu; sheria yako ndiyo furaha yangu.
175 Unijalie kuishi nipate kukusifu; na maagizo yako yanisaidie.
176 Natangatanga kama kondoo aliyepotea; uje kunitafuta mimi mtumishi wako, maana sikusahau amri zako.

Generic placeholder image