138

Sala ya shukrani
1 Nakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, kwa moyo wangu wote, naimba sifa zako mbele ya miungu.
2 Ninasujudu kuelekea hekalu lako takatifu; nalisifu jina lako, kwa sababu ya fadhili zako na uaminifu wako; kwa sababu umeweka jina lako na neno lako juu ya kila kitu.
3 Nilipokulilia, wewe ulinijibu; umeniongezea nguvu zangu.
4 Wafalme wote duniani watakusifu, ee Mwenyezi-Mungu, kwa sababu wameyasikia maneno yako.
5 Wataimba sifa za matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu, kwa maana utukufu wako ni mkuu.
6 Ingawa wewe ee Mwenyezi-Mungu, uko juu ya wote, unawaangalia kwa wema walio wanyonge; nao wenye kiburi huwaona kutoka mbali.
7 Hata nikikumbana na taabu, wewe wanilinda; waunyosha mkono wako dhidi ya hasira ya maadui zangu wakali; kwa nguvu yako kuu wanisalimisha.
8 Ee Mwenyezi-Mungu, utatimiza yote uliyoniahidi. Fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, zadumu milele. Usisahau kazi ya mkono wako mwenyewe.

Generic placeholder image