KITABU CHA NNE
(Zaburi 90–106)

90

Mungu wa milele na binadamu kiumbe
(Sala ya Mose, mtu wa Mungu)
1 Ee Bwana, tangu vizazi vyote, wewe umekuwa usalama wetu.
2 Kabla ya kuwapo milima, kabla hujauumba ulimwengu; wewe ndiwe Mungu, milele na milele.
3 Wamwambia binadamu, “Rudi mavumbini!” Naye binadamu hurudi mavumbini alimotoka!
4 Kwako miaka elfu ni kama siku moja tu, ni kama jana ambayo imekwisha pita; kwako ni kama mkesha mmoja wa usiku!
5 Wawafutilia mbali watu kama ndoto! Binadamu ni kama nyasi zinazochipua asubuhi:
6 Asubuhi huchipua na kuchanua, jioni zimekwisha nyauka na kukauka.
7 Hasira yako inatuangamiza; tunatishwa na ghadhabu yako.
8 Maovu yetu umeyaweka mbele yako; dhambi zetu za siri ziko wazi mbele yako.
9 Kwa hasira yako maisha yetu yatoweka, yanaisha kama pumzi.
10 Miaka ya kuishi ni sabini, au tukiwa wenye afya, themanini; lakini yote ni shida na taabu! Siku zapita mbio, nasi twatoweka mara!
11 Nani anayetambua uzito wa hasira yako? Nani anayejali matokeo ya ghadhabu yako?
12 Utufundishe ufupi wa maisha yetu ili tuweze kuwa na hekima.
13 Urudi, ee Mwenyezi-Mungu! Utakasirika hata lini? Utuonee huruma sisi watumishi wako.
14 Utushibishe fadhili zako asubuhi, tushangilie na kufurahi maisha yetu yote.
15 Utujalie sasa miaka mingi ya furaha, kama ulivyotupa miaka mingi ya shida na taabu.
16 Utuoneshe matendo yako sisi watumishi wako; uwaoneshe wazawa wetu uwezo wako mtukufu.
17 Utufadhili ee Bwana, Mungu wetu; uzitegemeze kazi zetu, uzifanikishe shughuli zetu.

Generic placeholder image