106

Wema wa Mungu kwa watu wake
1 Haleluya! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake zadumu milele!
2 Ni nani awezaye kutaja matendo ya Mwenyezi-Mungu? Ni nani awezaye kumsifu kama anavyostahili?
3 Heri wale wanaotekeleza haki, wanaotenda daima mambo yaliyo sawa.
4 Unikumbuke ee Mwenyezi-Mungu unapowafadhili watu wako; unisaidie wakati unapowaokoa;
5 ili niweze kuona fanaka ya wateule wako, nipate kufurahia furaha ya taifa lako, na kuona fahari pamoja na watu wako.
6 Tumetenda dhambi sisi na wazee wetu; tumetenda maovu, tumefanya mabaya.
7 Wazee wetu walipokuwa Misri, hawakujali matendo ya ajabu ya Mungu; hawakukumbuka wingi wa fadhili zake, bali walimwasi kando ya bahari ya Shamu.
8 Hata hivyo Mungu aliwaokoa kama alivyoahidi, ili aoneshe nguvu yake kuu.
9 Aliikemea bahari ya Shamu ikakauka; akawapitisha humo kama katika nchi kavu.
10 Aliwaokoa mikononi mwa waliowachukia; aliwaokoa kutoka kwa nguvu za maadui zao.
11 Maji ya bahari yaliwafunika maadui zao; wala hakusalia hata mmoja wao.
12 Hapo watu wake wakaamini maneno yake, wakamwimbia tenzi za sifa yake.
13 Lakini mara walisahau matendo yake, wakaacha kutegemea shauri lake.
14 Walijawa na tamaa kubwa kule jangwani, wakamjaribu Mungu kule nyikani.
15 Naye akawapa kile walichoomba, lakini akapeleka maradhi mabaya kati yao.
16 Kule kambini walimwonea wivu Mose, na Aroni mtumishi mtakatifu wa Mwenyezi-Mungu.
17 Ndipo ardhi ikafunguka ikammeza Dathani, na kumzika Abiramu na kundi lake lote;
18 moto ukawatokea wafuasi wao, ukawateketeza watu hao waovu.
19 Walitengeneza ndama wa dhahabu kule Horebu, wakaiabudu sanamu hiyo ya kusubu;
20 waliubadilisha utukufu wa Mungu, kwa sanamu ya mnyama ambaye hula nyasi.
21 Walimsahau Mungu aliyewaokoa, aliyetenda mambo makuu nchini Misri,
22 maajabu katika nchi hiyo ya Hamu, na mambo ya kutisha katika bahari ya Shamu.
23 Mungu alisema atawaangamiza watu wake, ila tu Mose mteule wake aliingilia kati, akaizuia hasira yake isiwaangamize.
24 Kisha wakaidharau nchi ile ya kupendeza, kwa sababu hawakuwa na imani na ahadi ya Mungu.
25 Walinungunika mahemani mwao, wala hawakumsikiliza Mwenyezi-Mungu.
26 Hivyo Mungu akainua mkono akaapa kwamba atawaangamizia jangwani;
27 atawatawanya wazawa wao kati ya watu, na kuwasambaza duniani kote.
28 Kisha wakajiunga kumwabudu Baali kule Peori, wakala tambiko zilizotambikiwa mizimu.
29 Waliichochea hasira ya Mwenyezi-Mungu kwa matendo yao, maradhi mabaya yakazuka kati yao.
30 Lakini Finehasi akasimama kufanya malipizi, na yale maradhi yakakoma.
31 Jambo hilo lakumbukwa kwa heshima yake, tangu wakati huo na nyakati zote.
32 Walimkasirisha Mungu penye maji ya Meriba, Mose akapata taabu kwa ajili yao.
33 Walimtia Mose uchungu rohoni, hata akasema maneno bila kufikiri.
34 Hawakuwaua watu wa mataifa mengine kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru.
35 Bali walijumuika na watu wa mataifa, wakajifunza kutenda mambo yao.
36 Waliabudu sanamu za miungu yao, nazo zikawa mtego wa kuwaangamiza.
37 Waliwaua watoto wao wa kiume na wa kike, wakawatoa tambiko kwa pepo.
38 Walimwaga damu ya wasio na hatia, damu ya watoto wao wa kiume na wa kike ambao waliwatoa tambiko kwa sanamu za Kanaani, nayo nchi ikatiwa unajisi kwa mauaji hayo.
39 Hivyo wakafanywa najisi kwa matendo yao, wakakosa uaminifu kwa Mungu kama wazinzi.
40 Hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawawakia watu wake, akachukizwa sana na hao waliokuwa mali yake.
41 Akawatia makuchani mwa watu wa mataifa, hao wenye kuwachukia wakawatawala.
42 Maadui zao waliwakandamiza, wakawatumikisha kwa nguvu.
43 Mara nyingi Mungu aliwaokoa watu wake, lakini wao wakachagua kumwasi, wakazidi kuzama katika uovu wao.
44 Hata hivyo Mungu alizijali taabu zao, wakati aliposikia kilio chao;
45 kwa ajili yao alilikumbuka agano lake, akawahurumia kwa wingi wa fadhili zake.
46 Aliwafanya waliowakandamiza wawaonee huruma.
47 Utuokoe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, utukusanye pamoja kutoka kwa mataifa, tupate kulisifu jina lako takatifu, na kuona fahari juu ya sifa zako.
48 Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele! Na watu wote waseme: “Amina!” Asifiwe Mwenyezi-Mungu!

Generic placeholder image