34

Sifa kwa wema wa Mungu
(Zaburi ya Daudi alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki)
1 Nitamtukuza Mwenyezi-Mungu nyakati zote, sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.
2 Mimi nitaona fahari juu ya Mwenyezi-Mungu, wanyonge wasikie na kufurahi.
3 Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu pamoja nami, sote pamoja tulisifu jina lake.
4 Nilimwomba Mwenyezi-Mungu naye akanijibu, na kuniondoa katika hofu zangu zote.
5 Mgeukieni Mungu mpate kufurahi; nanyi hamtaaibishwa kamwe.
6 Maskini alimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamsikia, na kumwokoa katika taabu zake zote.
7 Malaika wa Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wamchao, na kuwaokoa katika hatari.
8 Jaribuni mwone Mwenyezi-Mungu alivyo mwema. Heri mtu anayekimbilia usalama kwake.
9 Mcheni Mwenyezi-Mungu enyi watakatifu wake; maana wenye kumcha hawatindikiwi na kitu.
10 Hata wanasimba hutindikiwa na kuona njaa; lakini wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu hawakosi chochote chema.
11 Njoni enyi vijana mkanisikilize, nami nitawafundisha kumcha Mwenyezi-Mungu.
12 Je, watamani kufurahia maisha, kuishi maisha marefu na kufurahia mema?
13 Basi, acha kusema mabaya, na kuepa kusema uongo.
14 Jiepushe na uovu, utende mema; utafute amani na kuizingatia.
15 Mwenyezi-Mungu huwaangalia waadilifu, na kusikiliza malalamiko yao;
16 lakini huwapinga watu watendao maovu, awafutilie mbali kutoka duniani.
17 Waadilifu wakimlilia Mwenyezi-Mungu yeye huwasikia, na kuwaokoa katika taabu zao zote.
18 Mwenyezi-Mungu yu karibu na waliokufa moyo; huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.
19 Mateso ya mwadilifu ni mengi, lakini Mwenyezi-Mungu humwokoa kutoka yote.
20 Huvilinda viungo vya mwili wake wote, hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.
21 Ubaya huwaletea waovu kifo; wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.
22 Mwenyezi-Mungu huokoa maisha ya watumishi wake, wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.

Generic placeholder image