80

Maombi kwa ajili ya taifa
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yungiyungi. Zaburi ya Asafu)
1 Utege sikio, ewe Mchungaji wa Israeli, uwaongozaye wazawa wa Yosefu kama kondoo. Ewe ukaaye juu ya viumbe vyenye mabawa, uangaze,
2 mbele ya Efraimu, Benyamini na Manase. Uoneshe nguvu yako, uje kutuokoa!
3 Uturekebishe, ee Mungu; utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka.
4 Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, hata lini utazikasirikia sala za watu wako?
5 Umefanya huzuni iwe chakula chetu; umetunywesha machozi kwa wingi.
6 Umetufanya tuwe dharau kwa jirani zetu; maadui zetu wanatudhihaki.
7 Ee Mungu wa majeshi, uturekebishe, utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka.
8 Ulileta mzabibu kutoka Misri; ukawafukuza watu wa mataifa mengine, na kuupanda katika nchi yao.
9 Uliupalilia upate kukua, nao ukatoa mizizi na kuenea kote nchini.
10 Uliifunika milima kwa kivuli chake, na matawi yake yakawa kama mierezi mikubwa.
11 Matawi yake yalienea mpaka baharini; machipukizi yake mpaka kando ya mto Eufrate.
12 Mbona ulibomoa kuta zilizouzunguka? Sasa kila apitaye anachuma zabibu zake;
13 nguruwe mwitu wanauharibu, na wanyama wa porini wanautafuna!
14 Utugeukie tena ee Mungu wa majeshi. Uangalie toka mbinguni, uone; ukautunze mzabibu huo.
15 Uulinde mche ulioupanda kwa mkono wako; hilo chipukizi uliloimarisha wewe mwenyewe.
16 Watu walioukata na kuuteketeza, uwatazame kwa ukali, waangamie.
17 Mkono wako umkinge huyo uliyemfadhili; huyo uliyemteua kwa ajili yako.
18 Hatutakuacha na kukuasi tena; utujalie uhai, nasi tutakusifu.
19 Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi uturekebishe; utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka.

Generic placeholder image