47

Mungu, Mfalme wa ulimwengu wote
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi)
1 Enyi watu wote, pigeni makofi! Msifuni Mungu kwa sauti za shangwe!
2 Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu, anatisha. Yeye ni Mfalme mkuu wa ulimwengu wote.
3 Ametuwezesha kuwashinda watu wa mataifa, ameyaweka mataifa chini ya mamlaka yetu.
4 Ametuchagulia nchi hii iwe urithi wetu, ambayo ni fahari ya Yakobo anayempenda.
5 Mungu amepanda juu na vigelegele, Mwenyezi-Mungu na sauti ya tarumbeta.
6 Mwimbieni Mungu sifa, mwimbieni! Mwimbieni mfalme wetu sifa, mwimbieni!
7 Mwimbieni Mungu sifa kwa tenzi; maana yeye ni mfalme wa ulimwengu wote.
8 Mungu anayatawala mataifa yote; amekaa katika kiti chake cha enzi kitakatifu.
9 Viongozi wa watu wa mataifa wanakusanyika, wanajiunga na watu wa Mungu wa Abrahamu, maana nguvu zote duniani ni zake Mungu, yeye ametukuka sana.

Generic placeholder image