2

Mfalme mteule wa Mungu
1 Kwa nini mataifa yanafanya ghasia? Mbona watu wanafanya njama za bure?
2 Wafalme wa dunia wanajitayarisha; watawala wanashauriana pamoja, dhidi ya Mwenyezi-Mungu na mteule wake.
3 Wanasema: “Tujiondoe katika utawala wao; tutupilie mbali minyororo yao!”
4 Mwenyezi-Mungu atawalaye juu mbinguni, anawacheka na kuwadhihaki.
5 Kisha, anawakaripia kwa ghadhabu, na kuwatisha kwa hasira, akisema:
6 “Nimemtawaza mfalme niliyemteua, anatawala Siyoni, mlima wangu mtakatifu!”
7 Mfalme asema: “Nitatangaza azimio la Mwenyezi-Mungu. Mungu aliniambia: ‘Wewe ni mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako.
8 Niombe nami nitakupa mataifa yawe urithi wako, na dunia nzima kuwa mali yako.
9 Utawaponda kwa fimbo ya chuma; utawavunja kama chungu cha mfinyanzi!’”
10 Sasa enyi wafalme, tumieni busara; sikilizeni onyo hili, enyi watawala wa dunia.
11 Mtumikieni Mwenyezi-Mungu kwa uchaji;
12 msujudieni na kutetemeka; asije akakasirika, mkaangamia ghafla; kwani hasira yake huwaka haraka. Heri yao wote wanaokimbilia usalama kwake!

Generic placeholder image