135

Sifa kwa Mungu
1 Msifuni Mwenyezi-Mungu! Lisifuni jina la Mwenyezi-Mungu, msifuni enyi watumishi wake.
2 Msifuni enyi mkaao katika nyumba yake, ukumbini mwa nyumba ya Mungu wetu!
3 Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; mtukuzeni kwa nyimbo maana inafaa.
4 Mwenyezi-Mungu amemchagua Yakobo kuwa wake, nyinyi watu wa Israeli kuwa mali yake mwenyewe.
5 Najua hakika kuwa Mwenyezi-Mungu ni mkuu; Bwana wetu ni mkuu juu ya miungu yote.
6 Mwenyezi-Mungu hufanya chochote anachotaka, mbinguni, duniani, baharini na vilindini.
7 Ndiye aletaye mawingu kutoka mipaka ya dunia; afanyaye gharika kuu kwa umeme, na kuvumisha upepo kutoka ghala zake.
8 Ndiye aliyewaua wazaliwa wa kwanza huko Misri, wazaliwa wa watu na wanyama kadhalika.
9 Ndiye aliyefanya ishara na maajabu kwako, ee Misri, dhidi ya Farao na maofisa wake wote.
10 Ndiye aliyeyaangamiza mataifa mengi, akawaua wafalme wenye nguvu:
11 Kina Sihoni mfalme wa Waamori, Ogu mfalme wa Bashani, na wafalme wote wa Kanaani.
12 Alichukua nchi zao na kuwapa watu wake; naam, ziwe riziki ya watu wake Israeli.
13 Jina lako, ee Mwenyezi-Mungu, ladumu milele, utakumbukwa kwa fahari nyakati zote.
14 Mwenyezi-Mungu atawatetea watu wake; na kuwaonea huruma watumishi wake.
15 Miungu ya uongo ya mataifa ni fedha na dhahabu, imetengenezwa kwa mikono ya binadamu.
16 Ina vinywa, lakini haisemi; ina macho, lakini haioni.
17 Ina masikio, lakini haisikii; wala haiwezi hata kuvuta pumzi.
18 Wote walioifanya wafanane nayo, naam, kila mmoja anayeitegemea!
19 Enyi watu wa Israeli, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu! Enyi makuhani, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu!
20 Enyi Walawi, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu! Enyi wachaji wa Mwenyezi-Mungu, mtukuzeni!
21 Atukuzwe Mwenyezi-Mungu katika Siyoni, atukuzwe katika makao yake Yerusalemu. Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Generic placeholder image