38

Sala katika mateso
(Zaburi ya Daudi ya matoleo)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, usinikemee kwa hasira yako; usiniadhibu kwa ghadhabu yako.
2 Mishale yako imenichoma; mkono wako umenigandamiza.
3 Hamna mahali nafuu mwilini mwangu, kwa sababu umenikasirikia; hamna penye afya hata mifupani mwangu, kwa sababu ya dhambi yangu.
4 Nimefunikwa kabisa na dhambi zangu, zinanilemea kama mzigo mzito mno kwangu.
5 Madonda yangu yameoza na kunuka, na hayo ni matokeo ya ujinga wangu.
6 Nimepindika mpaka chini na kupondeka; mchana kutwa nazunguka nikiomboleza.
7 Viungo vyangu vimeshambuliwa na homa; mwilini mwangu hamna nafuu yoyote.
8 Nimelegea na kupondekapondeka; nasononeka kwa kusongwa moyoni.
9 Ee Bwana, wewe wajua tazamio langu lote; kwako hakikufichika kilio changu.
10 Moyo wanidunda, nguvu zimeniishia; hata macho yangu nayo yamekwisha fifia.
11 Rafiki na wenzangu wanaepa kuona mateso yangu, na jamaa zangu wanakaa mbali nami.
12 Wanaotaka kuniua wanatega mitego yao; wanaonitakia niumie wanatishia kuniangamiza. Mchana kutwa wanafanya mipango dhidi yangu.
13 Lakini mimi nimekuwa kama kiziwi, sisikii; nimekuwa kama bubu asiyeweza kusema kitu.
14 Naam, nimekuwa kama mtu asiyesikia, kama mtu asiye na chochote cha kujitetea.
15 Lakini ninakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu; wewe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, ndiwe utakayenijibu.
16 Nakuomba tu maadui wasinisimange, wasione fahari juu ya kuanguka kwangu.
17 Karibu sana nitaanguka; nakabiliwa na maumivu ya daima.
18 Naungama uovu wangu; dhambi zangu zanisikitisha.
19 Maadui zangu hawajambo, wana nguvu; ni wengi mno hao wanaonichukia bure.
20 Hao wanaonilipa maovu kwa wema wangu, wananipinga kwa sababu natenda mema.
21 Usinitupe, ee Mwenyezi-Mungu; ee Mungu wangu, usikae mbali nami.
22 Uje haraka kunisaidia; ewe Mwenyezi-Mungu, uliye wokovu wangu.

Generic placeholder image