112

Furaha ya mtu mwema
1 Msifuni Mwenyezi-Mungu! Heri mtu anayemcha Mwenyezi-Mungu, anayefurahia sana kutii amri zake.
2 Wazawa wake watakuwa wenye nguvu nchini; watoto wa wanyofu watapata baraka.
3 Nyumbani kwake kutakuwa na mali nyingi; uadilifu wake wadumu milele.
4 Mtu mwema huangaziwa mwanga gizani; mtu mwenye huruma, mpole na mwadilifu.
5 Mtu mkarimu akopeshaye bila faida, hufanikiwa; mtu afanyaye shughuli zake kwa kutumia haki.
6 Mwadilifu hatashindwa kamwe, huyo atakumbukwa milele.
7 Hana haja ya kuogopa akipata habari mbaya; ana moyo thabiti na humtegemea Mwenyezi-Mungu.
8 Yuko imara moyoni, wala hataogopa; naye atawaona maadui zake wanashindwa.
9 Hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini; uadilifu wake wadumu milele. Nguvu yake inatukuzwa kwa heshima.
10 Watu waovu huona hayo na kuudhika; husaga meno kwa chuki na kutoweka, matazamio ya mtu mbaya huishia patupu.

Generic placeholder image