111

Mungu asifika kwa matendo yake
1 Msifuni Mwenyezi-Mungu! Nitamshukuru Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote, nikijumuika na jamii ya watu waadilifu.
2 Matendo ya Mwenyezi-Mungu ni makuu mno! Wote wanaoyafurahia huyatafakari.
3 Kila afanyacho kimejaa utukufu na fahari; uadilifu wake wadumu milele.
4 Amesababisha matendo yake ya ajabu yakumbukwe; Mwenyezi-Mungu ni mwema na mwenye huruma.
5 Huwapa chakula wenye kumcha; hasahau kamwe agano lake.
6 Amewaonesha watu wake nguvu ya matendo yake, amewapa nchi za mataifa mengine ziwe mali yao.
7 Matendo yake ni ya haki na ya kuaminika; kanuni zake zote ni za kutegemewa.
8 Amri zake zadumu daima na milele; zimetolewa kwa haki na uadilifu.
9 Aliwakomboa watu wake na kufanya nao agano la milele. Yeye ni mtakatifu na wa kutisha mno!
10 Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa hekima; wote wanaozitii amri zake hujaliwa busara. Sifa zake zadumu milele.

Generic placeholder image