78

Mungu na watu wake
(Utenzi wa Asafu)
1 Sikieni mafundisho yangu, enyi watu wangu; yategeeni sikio maneno ya kinywa changu.
2 Nitasema nanyi kwa mafumbo, nitasema mambo yaliyofichika tangu kale;
3 mambo tuliyoyasikia na kuyajua, mambo ambayo wazee wetu walitusimulia.
4 Hatutawaficha watoto wetu; ila tutakisimulia kizazi kijacho matendo matukufu ya Mwenyezi-Mungu na uwezo wake; tutawaambia maajabu yake aliyotenda.
5 Aliwapa wazawa wa Yakobo masharti, aliweka sheria katika Israeli, ambayo aliwaamuru wazee wetu wawafundishe watoto wao;
6 ili watu wa kizazi kijacho, watoto watakaozaliwa baadaye, wazijue, nao pia wawajulishe watoto wao,
7 ili wamwekee Mungu tumaini lao, wasije wakasahau matendo ya Mungu, bali wazingatie amri zake.
8 Wasiwe kama walivyokuwa wazee wao, watu wakaidi na waasi; kizazi ambacho hakikuwa na msimamo thabiti, ambacho hakikuwa na uaminifu kwa Mungu.
9 Watu wa Efraimu, pinde na mishale mkononi, walirudi nyuma, wakakimbia siku ile ya vita.
10 Hawakulizingatia agano la Mungu; walikataa kufuata sheria yake.
11 Walisahau mambo aliyokuwa ametenda, miujiza aliyokuwa amewaonesha.
12 Alifanya maajabu mbele ya wazee wao, kondeni Soani, nchini Misri.
13 Aliigawa bahari, akawapitisha humo; aliyafanya maji yasimame kama ukuta.
14 Mchana aliwaongoza kwa wingu; usiku kucha kwa mwanga wa moto.
15 Aliipasua miamba kule jangwani, akawanywesha maji kutoka vilindini.
16 Alibubujisha vijito kutoka mwambani, akatiririsha maji kama mito.
17 Hata hivyo waliendelea kumkosea Mungu; walimwasi Mungu Mkuu kule jangwani.
18 Walimjaribu Mungu kwa makusudi; wakidai wapewe chakula walichotaka.
19 Walimkufuru Mungu wakisema: “Je, Mungu aweza kutupa chakula jangwani?
20 Ni kweli, aliupiga mwamba, maji yakabubujika kama mto; lakini, sasa aweza kweli kutupatia mkate, na kuwapatia watu wake nyama?”
21 Mwenyezi-Mungu, aliposikia hayo, alijawa na ghadhabu, moto ukawawakia wazawa wa Yakobo; hasira yake ikawavamia watu wa Israeli,
22 kwa sababu hawakuwa na imani naye, wala hawakuamini nguvu yake ya kuokoa.
23 Hata hivyo aliyaamuru mawingu ya juu, akaifungua milango ya mbingu;
24 akawanyeshea mana wale, akawapa nafaka kutoka mbinguni.
25 Binadamu, wakala chakula cha malaika; naye aliwapelekea chakula cha kutosha.
26 Alivumisha upepo wa mashariki, kwa nguvu yake akachochea pepo za kusini;
27 akawanyeshea watu wake nyama kama vumbi, ndege wengi kama mchanga wa pwani;
28 ndege hao walianguka kambini mwao, kila mahali kuzunguka makao yao.
29 Watu walikula wakashiba; Mungu aliwapa walichotaka.
30 Lakini hata kabla ya kutosheleza hamu yao, chakula kikiwa bado mdomoni mwao,
31 hasira ya Mungu iliwaka juu yao; akawaua wenye nguvu miongoni mwao, na kuwaangusha vijana wa Israeli.
32 Hata hivyo waliendelea kumkosea Mungu; ijapokuwa alitenda maajabu, hawakuamini.
33 Basi, akazikatisha siku zao kama pumzi, miaka yao kwa maafa ya ghafla.
34 Kila alipowaua, waliobaki walimgeukia; walitubu, wakamgeukia Mungu kwa moyo.
35 Walikumbuka kwamba Mungu alikuwa mwamba wao; Mungu Mkuu alikuwa mkombozi wao.
36 Lakini walimdanganya kwa maneno yao; kila walichomwambia kilikuwa uongo.
37 Hawakuambatana naye kwa moyo, hawakuwa waaminifu kwa agano lake.
38 Lakini Mungu mwenye huruma alisamehe uovu wao, na wala hakuwaangamiza. Mara nyingi aliizuia hasira yake, wala hakuiacha ghadhabu yake yote iwake.
39 Alikumbuka kwamba wao ni watu tu; ni kama upepo upitao na kutoweka.
40 Mara ngapi walimwasi kule jangwani, na kumchukiza hukohuko nyikani!
41 Walimjaribu Mungu tena na tena, wakamkasirisha huyo Mtakatifu wa Israeli.
42 Hawakuikumbuka nguvu yake, wala siku ile alipowaokoa na maadui zao,
43 alipotenda maajabu nchini Misri, na miujiza kondeni Soani!
44 Aliigeuza ile mito kuwa damu, Wamisri wasipate maji ya kunywa.
45 Aliwapelekea makundi ya nzi waliowasumbua, na vyura waliowatia hasara.
46 Alituma nzige, wakala mavuno yao, na kuharibu mashamba yao.
47 Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, na mitini yao kwa baridi kali.
48 Ngombe wao aliwaua kwa mvua ya mawe, na kondoo wao kwa radi.
49 Aliacha hasira yake kali iwawakie, ghadhabu, chuki na dhiki, na kundi la malaika waangamizi.
50 Aliachilia hasira yake iendelee, wala hakuwaepusha na kifo, bali aliwaangamiza kwa tauni.
51 Aliwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Wamisri; naam, chipukizi wa kwanza kambini mwa Hamu.
52 Kisha aliwahamisha watu wake kama kondoo, akawaongoza jangwani kama kundi la mifugo.
53 Aliwaogoza salama, wala hawakuogopa; lakini bahari iliwafunika maadui zao.
54 Aliwaleta katika nchi yake takatifu, katika mlima aliouteka kwa nguvu yake.
55 Aliyafukuza mataifa mbele yao, akazitoa nchi zao ziwe mali ya Israeli, akayakalisha makabila ya Israeli mahemani mwao.
56 Hata hivyo walimjaribu na kumwasi Mungu Mkuu; wala hawakuzingatia masharti yake.
57 Ila waligeuka na kufanya mabaya kama wazee wao; wakayumbayumba kama upinde usio imara.
58 Walimkasirisha kwa madhabahu zao za miungu; wakamchochea aone wivu kwa sanamu zao za kuchonga.
59 Mungu alipoona hayo, akawaka hasira; akamkataa Israeli katakata.
60 Aliyaacha makao yake kule Shilo, makao ambamo alikaa kati ya watu.
61 Aliiacha ishara ya nguvu yake itekwe, utukufu wake utiwe mikononi mwa maadui.
62 Aliwakasirikia watu wake mwenyewe; akawatoa waangamizwe kwa upanga.
63 Moto ukawateketeza vijana wao wa kiume, na wasichana wao wakakosa wachumba.
64 Makuhani wao walikufa kwa upanga, wala wajane wao hawakuomboleza.
65 Kisha Bwana aliamka kama kutoka usingizini, kama shujaa aliyechangamshwa na divai.
66 Akawatimua maadui zake; akawatia aibu ya kudumu milele.
67 Lakini aliikataa jamaa ya Yosefu, wala hakulichagua kabila la Efraimu.
68 Ila alilichagua kabila la Yuda, mlima Siyoni anaoupenda.
69 Alijenga hapo hekalu lake kubwa kama mbingu, kama dunia aliyoiweka imara milele.
70 Alimchagua Daudi, mtumishi wake, akamtoa katika kazi ya kuchunga kondoo.
71 Alimtoa katika kazi ya kuchunga kondoo na wanakondoo, awe na jukumu la kuchunga watu wa Yakobo taifa lake. Achunge Israeli, watu wake Mungu mwenyewe.
72 Daudi akawafunza kwa moyo wake wote, akawaongoza kwa uhodari mkubwa.

Generic placeholder image