29

Sauti ya Mungu katika dhoruba
(Zaburi ya Daudi)
1 Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima enyi viumbe vya mbinguni, semeni Mwenyezi-Mungu ni mtukufu na mwenye nguvu.
2 Semeni jina la Mwenyezi-Mungu ni tukufu. Mwabuduni katika mahali pake patakatifu.
3 Sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya maji; Mungu mtukufu angurumisha radi, sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya bahari!
4 Sauti ya Mwenyezi-Mungu ina nguvu, sauti ya Mwenyezi-Mungu imejaa fahari.
5 Sauti ya Mwenyezi-Mungu huvunja mierezi; Mwenyezi-Mungu avunja mierezi ya Lebanoni.
6 Huirusha milima ya Lebanoni kama ndama, milima ya Sirioni kama mwananyati.
7 Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutoa miali ya moto.
8 Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa, Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa la Kadeshi.
9 Sauti ya Mwenyezi-Mungu huitikisa mivule, hukwanyua majani ya miti msituni, na hekaluni mwake wote wasema: “Utukufu kwa Mungu!”
10 Mwenyezi-Mungu ameketi juu ya gharika; Mwenyezi-Mungu ni mfalme atawalaye milele.
11 Mwenyezi-Mungu na awape watu wake nguvu! Mwenyezi-Mungu na awabariki watu wake kwa amani!

Generic placeholder image