77

Faraja wakati wa shida
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Asafu)
1 Namlilia Mungu kwa sauti, kwa sauti namlilia Mungu anisikie.
2 Wakati wa taabu namwomba Bwana; namnyoshea mikono yangu usiku bila kuchoka, lakini sipati faraja yoyote kwa mtu.
3 Ninamfikiria Mungu na kusononeka; ninatafakari na kufa moyo.
4 Wanizuia hata kupata lepe la usingizi, nina mahangaiko hata kusema siwezi.
5 Nafikiria siku za zamani; nakumbuka miaka ya hapo kale.
6 Usiku nawaza na kuwazua moyoni; natafakari na kujiuliza rohoni:
7 “Je, Bwana ametuacha kabisa? Je, hatatuonesha tena hisani yake?
8 Je fadhili zake zimekoma kabisa? Je, hatatimiza tena ahadi zake?
9 Je, Mungu amesahau kuwa na huruma? Je, hasira yake imeuondoa upole wake?”
10 Kisha nikasema, “Kinachonichoma zaidi ni kwamba, Mungu Mkuu hatendi tena kitu kwa ajili yetu!”
11 Nitayakumbuka matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu, naam, nitayafikiria maajabu yako ya hapo kale.
12 Nitatafakari juu ya kazi zako, na kuwaza juu ya matendo yako makuu.
13 Kila ufanyacho ee Mungu, ni kitakatifu. Ni mungu gani aliye mkuu kama Mungu wetu?
14 Wewe ni Mungu unayetenda maajabu; wewe umeyaonesha mataifa uwezo wako.
15 Kwa mkono wako wa nguvu uliwakomboa watu wako; uliwakomboa wazawa wa Yakobo na Yosefu.
16 Maji yalipokuona, ee Mungu, maji yalipokuona, yaliogopa mno; naam, bahari ilitetemeka hata vilindini.
17 Mawingu yalichuruzika maji, ngurumo zikavuma angani, mishale ya umeme ikaangaza kila upande.
18 Kishindo cha ngurumo yako kilitokea katika kimbunga, umeme wako ukauangaza ulimwengu; dunia ikatikisika na kutetemeka.
19 Wewe uliweka njia yako juu ya bahari; ulitembea juu ya maji yale mengi, lakini nyayo zako hazikuonekana.
20 Uliwaongoza watu wako kama kondoo, chini ya uongozi wa Mose na Aroni.

Generic placeholder image