146

Sifa kwa Mungu Mwokozi
1 Msifuni Mwenyezi-Mungu! Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu!
2 Nitamsifu Mwenyezi-Mungu maisha yangu yote; nitamwimbia Mungu wangu muda wote niishipo.
3 Msiwategemee wakuu wa dunia; hao ni binadamu tu, hawawezi kuokoa.
4 Binadamu akitoa pumzi yake ya mwisho, anarudi mavumbini alimotoka; na hapo mipango yake yote hutoweka.
5 Heri mtu anayesaidiwa na Mungu wa Yakobo, mtu aliyeweka tumaini lake kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake,
6 aliyeumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo. Yeye hushika ahadi yake milele.
7 Yeye huwapatia wanaoonewa haki zao, huwapa wenye njaa chakula. Mwenyezi-Mungu huwapa wafungwa uhuru,
8 huwafungua macho vipofu. Mwenyezi-Mungu huwainua waliokandamizwa; huwapenda watu walio waadilifu.
9 Mwenyezi-Mungu huwalinda wageni, huwategemeza wajane na yatima; lakini huipotosha njia ya waovu.
10 Mwenyezi-Mungu atawala milele, Mungu wako, ee Siyoni, ni mfalme vizazi vyote! Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Generic placeholder image