140

Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe na watu wabaya, unikinge na watu wakatili.
2 Watu hao huwaza mabaya daima, huzusha magomvi kila mara.
3 Ndimi zao hatari kama za nyoka; midomoni mwao mna maneno ya sumu kama ya joka.
4 Ee Mwenyezi-Mungu, unilinde na makucha ya wabaya; unikinge na watu wakatili ambao wamepanga kuniangusha.
5 Wenye kiburi wamenitegea mitego, wametandaza kamba kama wavu, wameficha mitego njiani wanikamate.
6 Namwambia Mwenyezi-Mungu, “Wewe ndiwe Mungu wangu.” Usikilize, ee Mwenyezi-Mungu, sauti ya ombi langu.
7 Ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wangu, mkombozi wangu mkuu, umenikinga salama wakati wa vita.
8 Ee Mwenyezi-Mungu, usiwape waovu wanayotaka; wala mipango yao mibaya usiifanikishe.
9 Hao wanaonizingira wanainua vichwa; uovu wa maneno yao uwapate wao wenyewe!
10 Makaa ya moto yawaangukie; watumbukizwe mashimoni, wasiinuke tena.
11 Wanaowasengenya wengine wasifanikiwe katika nchi; uovu uwapate wakatili na kuwaangamiza mara!
12 Najua Mwenyezi-Mungu hutetea kisa cha wanaoteswa, na kuwapatia haki maskini.
13 Hakika waadilifu watalisifu jina lako; wanyofu watakaa kwako.

Generic placeholder image