132

Sifa ya nyumba ya Mungu
(Wimbo wa Kwenda Juu)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, mkumbuke Daudi, kumbuka taabu zote alizopata.
2 Ukumbuke ahadi aliyokupa, ee Mwenyezi-Mungu, kiapo alichokuapia, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo:
3 “Sitaingia ndani ya nyumba yangu, wala kulala kitandani mwangu;
4 sitakubali kulala usingizi, wala kusinzia;
5 mpaka nikupatie wewe Mwenyezi-Mungu mahali pa kukaa, makao yako, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo!”
6 Huko Efratha tulisikia habari za sanduku la agano, tukalikuta katika mashamba ya Yearimu.
7 “Haya! Twende nyumbani kwa Mungu, tuabudu mbele ya kiti chake cha enzi!”
8 Inuka ee Mwenyezi-Mungu, nenda kwenye maskani yako; inuka pamoja na sanduku la agano la uwezo wako!
9 Makuhani wako wawe waadilifu daima; na waaminifu wako wapige vigelegele vya furaha!
10 Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako, usimkatae huyo mfalme uliyemweka wakfu.
11 Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi kiapo thabiti, kiapo ambacho hatakibatilisha: “Nitamtawaza mmoja wa wazawa wako mwenyewe, kuwa mfalme baada yako.
12 Watoto wako wakishika agano langu, na kuzingatia mafundisho nitakayowapa, watoto wao pia watakuwa wafalme kama wewe.”
13 Mwenyezi-Mungu ameuchagua mji wa Siyoni, ametaka uwe makao yake:
14 “Hapa ndipo nitakapokaa milele, ndipo maskani yangu maana nimepachagua.
15 Nitaubariki sana mji wa Siyoni kwa mahitaji yake; nitawashibisha chakula maskini wake.
16 Nitawafanikisha makuhani wake kwa wokovu; waaminifu wake watapiga vigelegele vya furaha.
17 Humo nitamchipusha mfalme shujaa wa ukoo wa Daudi: Kama taa iwakayo nitamtegemeza mfalme niliyemteua.
18 Maadui zake nitawavika aibu; lakini yeye nitamvika fahari ya kifalme.”

Generic placeholder image