30

Sala ya shukrani
(Zaburi ya Daudi)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, nakutukuza maana umeniokoa, wala hukuwaacha maadui zangu wanisimange.
2 Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, nilikulilia msaada, nawe ukaniponya.
3 Ee Mwenyezi-Mungu, umeniokoa kutoka kuzimu; umenipa tena uhai, umenitoa miongoni mwa waendao kuzimu.
4 Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa, enyi waaminifu wake; kumbukeni utakatifu wake na kumshukuru.
5 Hasira yake hudumu kitambo kidogo, wema wake hudumu milele. Kilio chaweza kuwapo hata usiku, lakini asubuhi huja furaha.
6 Mimi nilipofanikiwa, nilisema: “Kamwe sitashindwa!”
7 Kwa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu, umeniimarisha kama mlima mkubwa. Lakini ukajificha mbali nami, nami nikafadhaika.
8 Nilikulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu; naam niliomba dua kwako ee Mwenyezi-Mungu:
9 “Je, utapata faida gani nikifa na kushuka hadi kwa wafu? Je, mavumbi ya wafu yanaweza kukusifu? Je, yanaweza kusimulia uaminifu wako?
10 Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, unihurumie; ee Mwenyezi-Mungu, unisaidie!”
11 Wewe umegeuza maombolezo langu kuwa ngoma ya furaha; umeniondolea huzuni yangu, ukanizungushia furaha.
12 Mimi nitakusifu wala sitakaa kimya. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu nitakushukuru milele.

Generic placeholder image