85

Kuliombea fanaka taifa
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, umeifadhili nchi yako; umemjalia Yakobo bahati nzuri tena.
2 Umewasamehe watu wako kosa lao; umezifuta dhambi zao zote.
3 Umeizuia ghadhabu yako yote; umeiacha hasira yako kali.
4 Uturekebishe tena, ee Mungu mwokozi wetu; uiondoe chuki uliyo nayo juu yetu.
5 Je, utatukasirikia hata milele? Je, utadumisha ghadhabu yako kwa vizazi vyote?
6 Je, hutatujalia tena maisha mapya, ili watu wako wafurahi kwa sababu yako?
7 Utuoneshe, fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, utujalie wokovu wako.
8 Hebu nisikie anachosema Mwenyezi-Mungu; maana anaahidi kuwapa watu wake amani, watu wake mwenyewe wasiporudia upuuzi wao
9 Hakika yu tayari kuwaokoa wanaomheshimu, na utukufu wake utadumu nchini mwetu.
10 Fadhili zake na uaminifu vitakutana; uadilifu na amani vitaungana.
11 Uaminifu utachipuka katika nchi; uadilifu utashuka toka mbinguni.
12 Naam, Mwenyezi-Mungu atatuletea fanaka, na nchi yetu itatoa mazao yake mengi.
13 Uadilifu utamtangulia Mungu na kumtayarishia njia yake.

Generic placeholder image