27

Kwa Mungu kuna usalama
(Zaburi ya Daudi)
1 Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu, ni nani nitakayemwogopa? Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu, sitamwogopa mtu yeyote.
2 Waovu wakinishambulia, na kutaka kuniangamiza, hao wapinzani wangu watajikwaa na kuanguka.
3 Hata jeshi likinizunguka, moyo wangu hautaogopa kitu; hata nikikabiliwa na vita, bado nitakuwa na tumaini.
4 Jambo moja nimemwomba Mwenyezi-Mungu, nalo ndilo ninalolitafuta: Nikae nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu siku zote za maisha yangu; niuone uzuri wake Mwenyezi-Mungu, na kutafuta maongozi yake hekaluni mwake.
5 Siku ya taabu atanificha bandani mwake; atanificha katika hema lake, na kunisalimisha juu ya mwamba.
6 Nami kwa fahari nitaangalia juu ya maadui zangu wanaonizunguka. Nitamtolea tambiko kwa shangwe hekaluni mwake, nitaimba na kumshangilia Mwenyezi-Mungu.

Msaada wapatikana kwa Mungu
7 Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, ninapokulilia, unionee huruma na kunijibu.
8 Moyo wangu waniambia: “Njoo umtafute Mungu!” Basi, naja kwako, ee Mwenyezi-Mungu.
9 Usiache kuniangalia kwa wema. Usinikatae kwa hasira mimi mtumishi wako; wewe umekuwa daima msaada wangu. Usinitupe wala usiniache, ee Mungu Mwokozi wangu.
10 Hata kama wazazi wangu wakinitupa, Mwenyezi-Mungu atanipokea kwake.
11 Unifundishe njia yako, ee Mwenyezi-Mungu; uniongoze katika njia iliyo sawa, kwa sababu ya maadui zangu.
12 Usiniache maadui wanitende wapendavyo; maana mashahidi wa uongo wananikabili, nao wanatoa vitisho vya ukatili.
13 Naamini nitauona wema wake Mwenyezi-Mungu katika makao ya walio hai.
14 Mtegemee Mwenyezi-Mungu! Uwe na moyo, usikate tamaa! Naam, mtegemee Mwenyezi-Mungu!

Generic placeholder image