46

Mungu yuko upande wetu
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi. Mtindo wa Alamothi)
1 Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu; yeye ni msaada wetu daima wakati wa taabu.
2 Kwa hiyo hatutaogopa chochote, dunia ijapoyeyuka na milima kutikisika kutoka baharini;
3 hata kama bahari ikichafuka na kutisha, na milima ikatetemeka kwa machafuko yake.
4 Kuna mto ambao maji yake hufurahisha mji wa Mungu, makao matakatifu ya Mungu Mkuu.
5 Mungu yumo mjini humo, nao hauwezi kutikiswa; Mungu ataupa msaada alfajiri na mapema.
6 Mataifa yaghadhibika na tawala zatikisika; Mungu anguruma nayo dunia yayeyuka.
7 Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.
8 Njoni mwone matendo ya Mwenyezi-Mungu; oneni maajabu aliyoyafanya duniani.
9 Hukomesha vita popote duniani, huvunjavunja pinde na mikuki, nazo ngao huziteketeza.
10 Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!”
11 Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.

Generic placeholder image