95

Utenzi wa kumsifu Mungu
1 Njoni tumwimbie Mwenyezi-Mungu, tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
2 Twende mbele zake na shukrani; tumshangilie kwa nyimbo za sifa.
3 Maana Mwenyezi-Mungu, ni Mungu mkuu; yeye ni Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
4 Vilindi vyote vya dunia vimo mikononi mwake, vilele vya milima ni vyake.
5 Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya; kwa mikono yake aliiumba nchi kavu.
6 Njoni tusujudu na kumwabudu; tumpigie magoti Mwenyezi-Mungu, Muumba wetu!
7 Maana yeye ni Mungu wetu, nasi ni watu wa kundi lake, ni kondoo wake anaowachunga. Laiti leo mngesikiliza sauti yake:
8 “Msiwe wakaidi kama kule Meriba, kama walivyokuwa kule Masa jangwani,
9 wazee wenu waliponijaribu na kunipima, ingawa walikuwa wameona mambo niliyowatendea.
10 Kwa miaka arubaini nilichukizwa nao, nikasema: ‘Kweli, hawa ni watu waliopotoka! Hawajali kabisa njia zangu!’
11 Basi, nilikasirika, nikaapa: ‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko!’”

Generic placeholder image