10

Sala dhidi ya udhalimu
1 Ee Mwenyezi-Mungu, mbona wasimama mbali? Kwa nini wajificha wakati tumo taabuni?
2 Kwa kiburi waovu wanawatesa maskini; njama zao ziwanase wao wenyewe.
3 Mwovu hujisifia tamaa zake mbaya, mtu wa tamaa hulaani na kumkataa Mwenyezi-Mungu.
4 Katika majivuno yake husema: “Mungu hatagundua.” Mawazo yake yote ni: “Hakuna Mungu.”
5 Njia za mwovu hufanikiwa daima; kwake hukumu zako ziko mbali na mawazo yake, na huwadharau maadui zake wote.
6 Huwaza moyoni: “Sitakuwa na wasiwasi; sitapatwa na dhiki maishani.”
7 Kinywa chake kimejaa laana, udanganyifu na dhuluma; mwepesi kusema maneno ya kuchukiza na maovu.
8 Hujificha vijijini huku anaotea, amuue kwa siri mtu asiye na hatia. Yuko macho kumvizia mnyonge;
9 huotea mafichoni mwake kama simba. Huvizia apate kuwakamata maskini; huwanasa kwa mtego wake na kuwachukua.
10 Mnyonge huvamiwa na kuangushwa chini; huangushwa kwa ukatili wa mtu mwovu.
11 Mwovu huwaza moyoni mwake: “Mungu amesahau; ameficha uso wake, haoni kitu!”
12 Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwaadhibu; usiwasahau wanaodhulumiwa.
13 Ee Mungu, kwa nini mwovu anakudharau, na kusema ati hutamfanya awajibike?
14 Lakini wewe wawaona wenye dhiki na shida; nawe daima uko tayari kuwasaidia. Mnyonge anakutegemea wewe, ee Mungu, wewe umekuwa daima msaada wa yatima.
15 Uzivunje nguvu za mtu mwovu; ukomeshe uovu wake wote, usiwepo tena.
16 Mwenyezi-Mungu ni mfalme milele na milele! Mataifa yasiyomjua yatatoweka nchini mwake.
17 Ee Mwenyezi-Mungu, wapokea dua za mnyonge; wampa moyo na kumtegea sikio.
18 Utawatendea haki yatima na wanaodhulumiwa, binadamu aliye udongo asiweze tena kuleta hofu.

Generic placeholder image