136

Wimbo wa shukrani
1 Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
2 Mshukuruni Mungu wa miungu; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
3 Mshukuruni Bwana wa mabwana; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
4 Ndiye peke yake atendaye makuu ya ajabu; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
5 Ndiye aliyeziumba mbingu kwa hekima; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
6 Ndiye aliyeitengeneza nchi juu ya vilindi vya maji; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
7 Ndiye aliyeumba jua, mwezi na nyota; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
8 Jua liutawale mchana; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
9 Mwezi na nyota vitawale usiku; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
10 Ndiye aliyewaua wazaliwa wa kwanza wa Misri; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
11 Akawaondoa watu wa Israeli kutoka huko; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
12 Kwa mkono wake wenye nguvu na enzi; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
13 Ndiye aliyeigawa Bahari ya Shamu sehemu mbili; kwa maana fadhili zake zadumu milele,
14 akawapitisha watu wa Israeli humo; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
15 Lakini akawazamisha humo Farao na jeshi lake; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
16 Ndiye aliyewaongoza watu wake jangwani; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
17 Ndiye aliyewapiga wafalme wenye nguvu; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
18 Akawaua wafalme maarufu; kwa maana fadhili zake zadumu milele;
19 akamuua Sihoni, mfalme wa Waamori, kwa maana fadhili zake zadumu milele;
20 na Ogu, mfalme wa Bashani; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
21 Akachukua nchi zao akawapa watu wake; kwa maana fadhili zake zadumu milele;
22 ziwe riziki ya Israeli, mtumishi wake; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
23 Ndiye aliyetukumbuka wakati wa unyonge wetu; kwa maana fadhili zake zadumu milele;
24 akatuokoa kutoka maadui zetu; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
25 Ndiye akipaye kila kiumbe chenye uhai chakula; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
26 Mshukuruni Mungu wa mbinguni; kwa maana fadhili zake zadumu milele!

Generic placeholder image