127

Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
(Wimbo wa Kwenda Juu, wa Solomoni)
1 Mwenyezi-Mungu asipoijenga nyumba, waijengao wanajisumbua bure. Mwenyezi-Mungu asipoulinda mji, waulindao wanakesha bure.
2 Mnajisumbua bure kuamka mapema asubuhi na kuchelewa kwenda kupumzika jioni, mjipatie chakula kwa jasho lenu. Mungu huwaruzuku walio wake hata walalapo.
3 Watoto ni riziki kutoka kwa Mwenyezi-Mungu; watoto ni tuzo lake kwetu sisi.
4 Watoto waliozaliwa wazazi wakiwa bado vijana, ni kama mishale mikononi mwa askari.
5 Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi. Hatashindwa atakapokabiliana na adui mahakamani.

Generic placeholder image