48

Siyoni mji wa Mungu
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi)
1 Mwenyezi-Mungu, ni mkuu; astahili kusifiwa sana katika mji wake na mlima wake mtakatifu.
2 Mlima Siyoni huko kaskazini, wapendeza kwa urefu; mji wa Mfalme mkuu ni furaha ya ulimwengu.
3 Mungu anazilinda ngome zake; yeye amejionesha kuwa ngome ya usalama.
4 Wafalme walikusanyika, wakaenda pamoja kushambulia.
5 Lakini walipouona mji wa Siyoni, wakashangaa; wakashikwa na hofu, wakatimua mbio.
6 Hofu kuu iliwashika, wakasikia uchungu kama mama anayejifungua,
7 kama waliokumbwa na kimbunga cha mashariki ambacho huzivunjavunja meli za Tarshishi.
8 Yote tuliyosikia tumejionea wenyewe katika mji wa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, naam, katika mji wa Mungu wetu; Mungu atauimarisha milele.
9 Ee Mungu, twazitafakari fadhili zako, tukiwa hekaluni mwako.
10 Jina lako lasifika kila mahali, sifa zako zaenea popote duniani. Kwa mkono wako umetenda kwa haki;
11 watu wa Siyoni na wafurahi! Watu wa Yuda na washangilie, kwa sababu ya maamuzi yako ya haki!
12 Tembeeni huko Siyoni mkauzunguke, mkaihesabu minara yake.
13 Zitazameni kuta zake na kuchunguza ngome zake; mpate kuvisimulia vizazi vijavyo, kwamba:
14 “Huyu ni Mungu, Mungu wetu milele! Atakuwa kiongozi wetu milele!”

Generic placeholder image