96

Mungu mfalme na hakimu
(1Nya 16:23-33)
1 Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya! Mwimbieni Mwenyezi-Mungu, ulimwengu wote!
2 Mwimbieni Mwenyezi-Mungu na kulisifu jina lake. Tangazeni kila siku matendo yake ya wokovu.
3 Yatangazieni mataifa utukufu wake, waambieni watu wote matendo yake ya ajabu.
4 Maana Mwenyezi-Mungu ni mkuu, anasifika sana; anastahili kuheshimiwa kuliko miungu yote.
5 Miungu ya mataifa mengine si kitu; lakini Mwenyezi-Mungu aliziumba mbingu.
6 Utukufu na fahari vyamzunguka; nguvu na uzuri vyalijaza hekalu lake.
7 Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima, enyi jamii zote za watu; naam, kirini utukufu na nguvu yake.
8 Lisifuni jina lake tukufu; leteni tambiko na kuingia hekaluni mwake.
9 Mwabuduni Mwenyezi-Mungu katika patakatifu pake; tetemekeni mbele yake ee dunia yote!
10 Yaambieni mataifa: “Mwenyezi-Mungu anatawala! Ameuweka ulimwengu imara, hautatikisika. Atawahukumu watu kwa haki!”
11 Furahini enyi mbingu na dunia! Bahari na ivume pamoja na vyote vilivyomo!
12 Furahini enyi mashamba na vyote vilivyomo! Ndipo miti yote misituni itaimba kwa furaha,
13 mbele ya Mwenyezi-Mungu anayekuja; naam, anayekuja kuihukumu dunia. Ataihukumu dunia kwa haki, na mataifa kwa uaminifu wake.

Generic placeholder image