89

Wakati wa taabu ya kitaifa
(Utenzi wa Ethani Mwezrahi)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, nitaimba fadhili zako milele; nitavitangazia vizazi vyote uaminifu wako.
2 Natamka kuwa fadhili zako zadumu milele; uaminifu wako ni thabiti kama mbingu.
3 Umesema: “Nimefanya agano na mteule wangu, nimemwapia mtumishi wangu Daudi:
4 ‘Daima nitamweka mzawa wako kuwa mfalme, tena nitaudumisha ufalme wako milele.’”
5 Mbingu na zisifu maajabu yako, ee Mwenyezi-Mungu; uaminifu wako usifiwe katika kusanyiko la watakatifu.
6 Nani mbinguni awezaye kulinganishwa nawe ee Mwenyezi-Mungu? Nani aliye sawa nawe kati ya viumbe vya mbinguni?
7 Wewe waogopwa katika baraza la watakatifu; wote wanaokuzunguka wanatiwa hofu kuu.
8 Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, ni nani mwenye nguvu kama wewe, ee Mwenyezi-Mungu? Uaminifu umekuzunguka pande zote.
9 Wewe watawala machafuko ya bahari; mawimbi yake yakiinuka, wayatuliza.
10 Uliliponda joka Rahabu na kuliua; uliwatawanya adui zako kwa nguvu yako.
11 Mbingu ni zako na dunia ni yako pia; ulimwengu na vitu vyote vilivyomo wewe uliviumba.
12 Wewe uliumba kaskazini na kusini; milima Tabori na Hermoni inakusifu kwa furaha.
13 Mkono wako una nguvu, mkono wako una nguvu na umeshinda!
14 Uadilifu na haki ni msingi wa utawala wako; fadhili na uaminifu vyakutangulia!
15 Heri watu wanaojua kukushangilia, wanaoishi katika mwanga wa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu.
16 Wanafurahi mchana kutwa kwa sababu yako, na kukusifu kwa ajili ya uadilifu wako.
17 Wewe ndiwe fahari na nguvu yao; kwa wema wako twapata ushindi.
18 Ee Mwenyezi-Mungu, mlinzi wetu ni wako, mfalme wetu ametoka kwako ewe Mtakatifu wa Israeli.

Ahadi ya Mungu kwa Daudi
19 Zamani ulinena katika maono, ukawaambia watumishi wako waaminifu: “Nimempa nguvu shujaa mmoja, nimemkuza huyo niliyemteua kati ya watu.
20 Nimempata Daudi, mtumishi wangu; nimemweka wakfu kwa mafuta yangu matakatifu.
21 Mkono wangu wa nguvu utakuwa naye daima; mkono wangu mimi mwenyewe utamwimarisha.
22 Maadui hawataweza kumshinda, wala waovu hawatamnyanyasa.
23 Mimi nitawaponda wapinzani wake; nitawaangamiza wote wanaomchukia.
24 Nitakuwa mwaminifu kwake na kumfadhili, kwa jina langu atapata ushindi mkubwa.
25 Nitaimarisha nguvu na utawala wake, toka bahari hata mito.
26 Yeye ataniita: ‘Wewe ni Baba yangu, Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu.’
27 Nami nitamfanya kuwa mzaliwa wangu wa kwanza, mkuu kuliko wafalme wote duniani.
28 Fadhili zangu nitamwekea milele, na agano langu kwake litadumu daima.
29 Nitaudumisha daima ukoo wake wa kifalme, na ufalme wake kama mbingu.
30 “Lakini wazawa wake wakiiacha sheria yangu, wasipoishi kadiri ya maagizo yangu,
31 kama wakizivunja kanuni zangu, na kuacha kutii amri zangu,
32 hapo nitawaadhibu makosa yao; nitawapiga kwa sababu ya uovu wao.
33 Lakini sitaacha kumfadhili Daudi, wala kuwa mwongo kuhusu uaminifu wangu.
34 Sitavunja agano langu naye, wala kubatili neno nililotamka kwa mdomo wangu.
35 “Nimeapa mara moja tu kwa utakatifu wangu; nami sitamwambia Daudi uongo.
36 Ukoo wake utadumu milele; na ufalme wake kama jua.
37 Utadumu milele kama mwezi utokezavyo angani.”

Majonzi ya sasa
38 Lakini sasa ee Mungu, umemtupa na kumkataa, umejaa ghadhabu dhidi ya huyo uliyemweka wakfu.
39 Umefuta agano ulilofanya na mtumishi wako; umeitupa taji yake mavumbini.
40 Kuta zote za mji wake umezibomoa; ngome zake umezivunjavunja.
41 Wote wapitao wanampokonya mali zake; amekuwa dharau kwa jirani zake.
42 Maadui zake umewapa ushindi; umewafurahisha maadui zake wote.
43 Silaha zake umezifanya butu; ukamwacha ashindwe vitani.
44 Umemvua madaraka yake ya kifalme ukauangusha chini utawala wake.
45 Umezipunguza siku za ujana wake, ukamfunika fedheha tele.

Kuomba usalama
46 Ee Mwenyezi-Mungu, utajificha hata milele? Hata lini hasira yako itawaka kama moto?
47 Ukumbuke, ee Bwana, ufupi wa maisha yangu; kwamba binadamu uliyemuumba anaishi muda mfupi!
48 Ni mtu gani aishiye asipate kufa? Nani awezaye kujiepusha na kifo?
49 Ee Bwana, ziko wapi basi fadhili zako, ulizomwapia Daudi kwa uaminifu wako?
50 Ee Bwana, ukumbuke anavyotukanwa mtumishi wako, jinsi nivumiliavyo matusi ya wasiokujua.
51 Ona wanavyomzomea, ee Mwenyezi-Mungu; jinsi wanavyomdhihaki mteule wako kila aendako.
52 Asifiwe Mwenyezi-Mungu milele! Amina! Amina!

Generic placeholder image