142

Dua ya mtu aliyeachwa mpweke
(Utenzi wa Daudi alipokuwa pangoni. Sala)
1 Namlilia Mwenyezi-Mungu kwa sauti, namsihi Mwenyezi-Mungu kwa sauti yangu.
2 Namwekea malalamiko yangu, namweleza taabu zangu.
3 Ninapokaribia kukata tamaa kabisa, yeye yupo, anajua mwenendo wangu. Maadui wamenitegea mitego njiani mwangu.
4 Nikiangalia upande wa kulia na kungojea, naona hakuna mtu wa kunisaidia; sina tena mahali pa kukimbilia, hakuna mtu anayenijali.
5 Nakulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu! Wewe ni kimbilio langu la usalama; wewe ni riziki yangu kuu katika nchi ya walio hai.
6 Usikilize kilio changu, maana nimekuwa hoi; uniokoe na watesi wangu, maana wamenizidi nguvu.
7 Unitoe humu kifungoni, ili nipate kukushukuru. Watu waadilifu watajiunga nami kwa sababu umenitendea mema mengi.

Generic placeholder image