101

Mwongozo mzuri wa mfalme
(Zaburi ya Daudi)
1 Utenzi wangu kuhusu uaminifu na haki; ninauimba kwa heshima yako, ee Mwenyezi-Mungu.
2 Nitazingatia mwenendo usio na hatia. Je, utakuja kwangu lini? Nitaishi kwa unyofu nyumbani kwangu;
3 sitavumilia kamwe upuuzi. Nayachukia matendo ya watu wapotovu, mambo yao hayataambatana nami.
4 Upotovu wowote ule uwe mbali nami; sitahusika kabisa na uovu.
5 Anayemsengenya jirani nitamfutilia mbali; sitamvumilia mwenye majivuno na kiburi.
6 Nitawaangalia kwa wema watu walio waaminifu, wapate kuishi pamoja nami. Watu wanyofu ndio watakaonitumikia.
7 Mwongo yeyote hatakaa nyumbani mwangu; hakuna msema uongo atakayekaa kwangu.
8 Siku kwa siku nitawaangamiza waovu wote nchini; nitawaangamiza wabaya wote mjini mwa Mwenyezi-Mungu.

Generic placeholder image