41

Sala ya mgonjwa
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1 Heri mtu anayewajali maskini; Mwenyezi-Mungu atamwokoa wakati wa shida.
2 Mwenyezi-Mungu atamlinda na kumweka hai, naye atafanikiwa katika nchi; Mungu hatamwacha makuchani mwa maadui zake.
3 Mwenyezi-Mungu atamsaidia awapo mgonjwa, atamponya maradhi yake yote.
4 Nami nilisema: “Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu, unihurumie maana nimekukosea wewe.”
5 Madui zangu husema vibaya juu yangu: “Atakufa lini na jina lake litoweke!”
6 Wanitembeleapo husema maneno matupu; wanakusanya mabaya juu yangu, na wafikapo nje huwatangazia wengine.
7 Wote wanichukiao hunongonezana juu yangu; wananiwazia mabaya ya kunidhuru.
8 Husema: “Maradhi haya yatamuua; hatatoka tena kitandani mwake!”
9 Hata rafiki yangu wa moyoni niliyemwamini, rafiki ambaye alishiriki chakula changu, amegeuka kunishambulia!
10 Ee Mwenyezi-Mungu, unionee huruma! Unipe nafuu, nami nitawalipiza.
11 Hivyo nitajua kwamba unapendezwa nami, maadui zangu wasipopata fahari juu yangu.
12 Wewe umenitegemeza kwani natenda mema; waniweka mbele yako milele.
13 Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele! Amina! Amina!

Generic placeholder image