62

Mungu mlinzi wangu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi)
1 Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu, kwake watoka wokovu wangu.
2 Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika.
3 Hata lini mtanishambulia mimi? Hata lini nyinyi nyote mtanipiga, mimi niliye kama kiambaza kilichoinama, kama ukuta unaoanza kubomoka?
4 Mmepanga kuniangusha toka mahali pangu pa heshima; furaha yenu ni kusema uongo. Kwa maneno, mnabariki, lakini moyoni mnalaani.
5 Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu; kwake naliweka tumaini langu.
6 Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika.
7 Wokovu na fahari yangu vyatoka kwa Mungu; mwamba wangu mkuu na kimbilio langu ni Mungu.
8 Enyi watu, mtumainieni Mungu daima; mfungulieni Bwana yaliyo moyoni mwenu. Mungu ndiye kimbilio la usalama wetu.
9 Binadamu wote ni kama pumzi tu; wote, wakubwa kwa wadogo, hawafai kitu. Tena ukiwapima uzito hawafikii kilo, wote pamoja ni wepesi kuliko pumzi.
10 Msitegemee dhuluma, msijisifie mali ya wizi; kama mali zikiongezeka, msizitegemee.
11 Mungu ametamka mara moja, nami nimesikia tena na tena: Kwamba enzi ni mali yake Mungu;
12 naam, nazo fadhili ni zake Bwana; humlipa kila mtu kadiri ya matendo yake.

Generic placeholder image