79

Wakati wa maafa ya taifa
(Zaburi ya Asafu)
1 Ee Mungu, watu wasiokujua wameivamia nchi yako. Wamelitia najisi hekalu lako takatifu, na kuufanya mji wa Yerusalemu kuwa magofu.
2 Wameacha maiti za watumishi wako ziliwe na ndege, miili ya watu wako chakula cha wanyama wa porini.
3 Damu yao imemwagwa kama maji mjini Yerusalemu, wamelazwa humo na hakuna wa kuwazika.
4 Tumekuwa aibu kwa mataifa ya jirani, jirani zetu wanatucheka na kutudhihaki.
5 Ee Mwenyezi-Mungu, je, utakasirika hata milele? Hasira yako ya wivu itawaka kama moto hata lini?
6 Uwamwagie watu wasiokujua hasira yako; naam, tawala zote zisizoheshimu jina lako.
7 Maana wamemmeza Yakobo, taifa lako, wameteketeza kabisa makao yake.
8 Usituadhibu kwa sababu ya makosa ya wazee wetu. Huruma yako itujie haraka, maana tumekandamizwa mno!
9 Utusaidie, ee Mungu, mwokozi wetu; kwa heshima ya jina lako utuokoe na kutusamehe dhambi zetu, kwa ajili ya jina lako.
10 Kwa nini mataifa yatuambie: “Yuko wapi Mungu wenu?” Utujalie tuone ukiwalipiza watu wa mataifa mauaji ya watumishi wako.
11 Kilio cha hao wafungwa kikufikie; kwa nguvu yako kuu uwaokoe waliohukumiwa kufa.
12 Mataifa hayo yaliyokudharau, ee Bwana, yalipizwe mara saba!
13 Nasi watu wako, tulio kondoo wa kundi lako, tutakushukuru milele, na kukusifu nyakati zote.

Generic placeholder image