49

Upumbavu wa kutegemea mali
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi)
1 Sikieni jambo hili enyi watu wote! Tegeni sikio enyi wakazi wote wa dunia;
2 sikilizeni nyote, wakubwa kwa wadogo, matajiri na maskini kwa pamoja.
3 Maneno yangu yatakuwa mazitomazito; mimi nitasema maneno ya hekima.
4 Nitatega sikio nisikilize methali, nitafafanua kitendawili kwa muziki wa zeze.
5 Ya nini niogope siku mbaya, wakati nizungukwapo na uovu wa adui?
6 Watu waovu hutegemea mali zao, hujisifia wingi wa utajiri wao.
7 Lakini binadamu hawezi kamwe kujikomboa mwenyewe; hawezi kumlipa Mungu bei ya maisha yake,
8 maana fidia ya maisha ni kubwa mno. Hawezi kutoa kitu chochote kinachotosha,
9 kimwezeshe aendelee kuishi daima, asipate kuonja kaburi.
10 Yeye afahamu kuwa hata wenye hekima hufa, wapumbavu hali kadhalika na watu wajinga. Wote hao huwaachia wengine mali zao.
11 Makaburi ni makao yao hata milele; ni makao yao vizazi hata vizazi, ingawa hapo awali walimiliki ardhi.
12 Binadamu hatadumu katika fahari yake; atakufa tu kama mnyama.
13 Hayo ndiyo yawapatao wanaojiamini kipumbavu, ndio mwisho wa wale wanaojivunia mali zao.
14 Wataongozwa kama kondoo hadi kuzimu, kifo kitakuwa mchungaji wao. Watashuka moja kwa moja kaburini. Miili yao itaozea huko, Kuzimu kutakuwa makao yao.
15 Lakini Mungu ataniokoa na kuzimu. Atanisalimisha kutoka huko.
16 Usihangaike ukiona mtu anatajirika, wala mali yake ikiongezeka zaidi na zaidi.
17 Maana atakapokufa hatachukua chochote, mali yake haitashuka huko chini pamoja naye.
18 Ajapojikuza katika maisha haya, na kusifiwa kwa sababu ya kufanikiwa,
19 atajiunga na wazee waliomtangulia kufa, ambao hawawezi kuona tena mwanga.
20 Binadamu hatadumu milele katika fahari yake, atakufa tu kama mnyama.

Generic placeholder image