81

Wimbo wa sikukuu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Gitithi. Zaburi ya Asafu)
1 Mwimbieni kwa sauti Mungu, nguvu yetu, mshangilieni Mungu wa Yakobo;
2 vumisheni wimbo wa shangwe, pigeni ngoma, chezeni zeze na kinubi cha sauti nzuri.
3 Pigeni tarumbeta kutangaza mwezi mwandamo, na pia mwezi mpevu, wakati wa sikukuu yetu.
4 Hiyo ndiyo kanuni katika Israeli; hilo ndilo agizo la Mungu wa Yakobo.
5 Aliwapa watu wa Israeli agizo hilo, alipoishambulia nchi ya Misri. Nasikia sauti nisiyoitambua ikisema:
6 “Mimi nilikutua mizigo yako mabegani, nilikuondolea matofali uliyochukua mikononi.
7 Ukiwa shidani uliniita, nami nikakuokoa. Nilikujibu nikiwa mafichoni katika ngurumo. Nilikujaribu kwenye maji ya Meriba.
8 Enyi watu wangu, sikieni onyo langu. Laiti ungenisikiliza, ee Israeli!
9 Asiwepo kwako mungu wa kigeni; usiabudu kamwe mungu mwingine.
10 Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri. Fumbua kinywa chako, nami nitakulisha.
11 “Lakini watu wangu hawakunisikiliza; Israeli hakunitaka kabisa.
12 Hivyo, nikawaacha wabaki na ukaidi wao; wafuate mashauri yao wenyewe.
13 Laiti watu wangu wangenisikiliza! Laiti Israeli angefuata njia yangu!
14 Ningewashinda maadui zao haraka; ningenyosha mkono dhidi ya wadhalimu wao.
15 Wanichukiao wangenipigia magoti kwa hofu, na adhabu yao ingekuwa ya milele.
16 Lakini wewe ningekulisha kwa ngano bora, ningekushibisha kwa asali ya mwambani.”

Generic placeholder image