143

Sala ya kuomba msaada
(Zaburi ya Daudi)
1 Usikie sala yangu, ee Mwenyezi-Mungu! Ulitegee sikio ombi langu maana wewe ni mwaminifu; unijibu kwa sababu ya uadilifu wako.
2 Usinitie hukumuni mimi mtumishi wako, maana hakuna yeyote aliye mwadilifu mbele yako.
3 Maadui zangu wamenifuatia; wameniangusha chini kabisa wameniketisha gizani kama mtu aliyekufa zamani.
4 Nimevunjika moyo kabisa; nimekufa ganzi kwa ajili ya woga.
5 Nakumbuka siku zilizopita; natafakari juu ya yote uliyotenda, nawaza na kuwazua juu ya matendo yako.
6 Nakunyoshea mikono yangu kuomba; nina kiu yako kama nchi kavu isiyo na maji.
7 Ee Mwenyezi-Mungu, unijibu haraka; maana nimekata tamaa kabisa! Usijifiche mbali nami, nisije nikawa kama wale washukao kwa wafu.
8 Asubuhi unioneshe fadhili zako, maana nimekuwekea tumaini langu. Unifundishe mwenendo wa kufuata, maana nakuelekezea ombi la moyo wangu.
9 Uniokoe, ee Mwenyezi-Mungu, kutoka maadui zangu, maana kwako nakimbilia usalama.
10 Unifundishe kutimiza matakwa yako, maana wewe ni Mungu wangu! Roho yako nzuri iniongoze katika njia sawa.
11 Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu, kwa hisani yako, uniondoe katika taabu kwa sababu ya uadilifu wako.
12 Kwa sababu ya fadhili zako uwakomeshe maadui zangu, uwaangamize wote wanaonidhulumu; maana mimi ni mtumishi wako.

Generic placeholder image