114

Mungu na watu wake
1 Watu wa Israeli walipotoka Misri, wazawa wa Yakobo walipotoka ugenini,
2 Yuda ikawa maskani ya Mungu, Israeli ikawa milki yake.
3 Bahari iliona hayo ikakimbia; mto Yordani ukaacha kutiririka!
4 Milima ilirukaruka kama kondoo dume; vilima vikaruka kama wanakondoo!
5 Ee bahari, imekuwaje hata ukakimbia? Nawe Yordani, kwa nini ukaacha kutiririka?
6 Enyi milima, mbona mliruka kama kondoo dume? Nanyi vilima, mmerukaje kama wanakondoo?
7 Tetemeka, ee dunia mbele yake Mwenyezi-Mungu; tetemeka mbele ya Mungu wa Yakobo,
8 anayeugusa mwamba ukawa bwawa la maji, nayo majabali yakawa chemchemi za maji!

Generic placeholder image