32

Maondoleo ya dhambi
(Zaburi ya Daudi. Funzo)
1 Heri yake mtu aliyesamehewa kosa lake, mtu ambaye dhambi yake imeondolewa kabisa.
2 Heri mtu ambaye Mwenyezi-Mungu hamwekei hatia, mtu ambaye hana hila moyoni mwake.
3 Wakati nilipokuwa sijakiri dhambi yangu, nilikuwa nimedhoofika kwa kulia mchana kutwa.
4 Mchana na usiku mkono wako ulinilemea; nikafyonzwa nguvu zangu, kama maji wakati wa kiangazi.
5 Kisha nilikiri makosa yangu kwako; wala sikuuficha uovu wangu. Nilisema ninakuungamia makosa yangu ee Mwenyezi-Mungu, ndipo nawe ukanisamehe dhambi zangu zote.
6 Kwa hiyo, kila mwaminifu na akuletee maombi; jeshi likaribiapo au mafuriko, hayo hayatamfikia yeye.
7 Wewe ndiwe kinga yangu; wewe wanilinda katika taabu. Umenijalia shangwe za kukombolewa.
8 Mungu asema: “Nitakufunza na kukuonesha njia unayopaswa kufuata. Nitakushauri kwa uangalifu mkubwa.
9 Usiwe mpumbavu kama farasi au nyumbu, ambao lazima wafungwe lijamu na hatamu, la sivyo hawatakukaribia.”
10 Watu waovu watapata mateso mengi, bali wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu wazungukwa na fadhili zake.
11 Furahini na kushangilia kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu; pigeni vigelegele vya shangwe enyi wanyofu wa moyo.

Generic placeholder image