44

Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
(Kwa Mwimbishaji. Utenzi wa Wakorahi)
1 Ee Mungu, sisi tumesikia kwa masikio yetu, wazee wetu wametusimulia mambo uliyotenda nyakati zao, naam, mambo uliyotenda hapo kale:
2 Kwa mkono wako mwenyewe uliyafukuza mataifa mengine, na mahali pao ukawakalisha watu wako; uliyaadhibu mataifa mengine, na kuwafanikisha watu wako.
3 Watu wako hawakuitwaa nchi kwa silaha zao, wala hawakupata ushindi kwa nguvu zao; ila uliwasalimisha kwa mkono wako mwenyewe, kwa kuwaangazia uso wako, kwani wewe uliwapenda.
4 Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu! Wawajalia ushindi wazawa wa Yakobo.
5 Kwa nguvu yako twawashinda maadui zetu, kwa jina lako twawakanyaga wanaotushambulia.
6 Mimi siutegemei upinde wangu, wala upanga wangu hauwezi kuniokoa.
7 Wewe ndiwe uliyetuokoa na maadui zetu; uliwavuruga wale waliotuchukia.
8 Daima tutaona fahari juu yako, ee Mungu; tutakutolea shukrani milele.
9 Lakini sasa umetuacha na kutufedhehesha; huandamani tena na majeshi yetu.
10 Umetufanya tuwakimbie maadui zetu, nao wakaziteka nyara mali zetu.
11 Umetufanya kama kondoo wanaopelekwa kuchinjwa; umetutawanya kati ya mataifa mengine.
12 Umewauza watu wako kwa bei ya chini; wala hukupata faida yoyote.
13 Umetufanya kuwa kioja kwa jirani zetu, nao wanatudhihaki na kutucheka.
14 Umetufanya tudharauliwe na watu wa mataifa; wanatutikisia vichwa vyao kwa kutupuuza.
15 Mchana kutwa fedheha yaniandama, na uso wangu umejaa aibu tele
16 kwa maneno na madharau ya wenye kunitukana, kwa kukabiliwa na maadui zangu na walipiza kisasi.
17 Hayo yote yametupata sisi ijapokuwa hatujakusahau, wala hatujavunja agano lako.
18 Hatujakuasi wewe, wala hatujaziacha njia zako.
19 Hata hivyo umetuacha hoi kati ya wanyama wakali; umetuacha katika giza kuu.
20 Tungalikuwa tumekusahau wewe Mungu wetu, tukamkimbilia mungu wa uongo,
21 ee Mungu, ungalikwisha jua jambo hilo, kwa maana wewe wazijua siri za moyoni.
22 Lakini kwa ajili yako twakikabili kifo kila siku; tunatendewa kama kondoo wanaopelekwa kuchinjwa.
23 Amka, ee Bwana! Mbona umelala? Inuka! Tafadhali usitutupe milele!
24 Mbona wajificha mbali nasi, na kusahau dhiki na mateso yetu?
25 Tumedidimia hata mavumbini, tumegandamana na ardhi.
26 Uinuke, uje kutusaidia! Utukomboe kwa sababu ya fadhili zako.

Generic placeholder image