59

Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Usiharibu”. Utenzi wa Daudi wakati Shauli alipotuma wapelelezi wamuue)
1 Ee Mungu wangu, uniokoe na maadui zangu; unikinge na hao wanaonishambulia.
2 Uniokoe na hao wanaotenda maovu; unisalimishe kutoka kwa hao wauaji!
3 Tazama! Wananivizia waniue; watu wakatili wanachochea ugomvi dhidi yangu.
4 Bila ya kosa, hatia au dhambi yangu, wanakimbia, ee Mwenyezi-Mungu, kujiweka tayari. Uinuke, ee Mwenyezi-Mungu, ukatazame na kunisaidia!
5 Uinuke, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu Mwenye Nguvu, Mungu wa Israeli. Uamke, uwaadhibu hao watu wasiokujua; usiwaache hao wanaopanga ubaya.
6 Kila jioni maadui hao hurudi wakibweka kama mbwa, na kuzungukazunguka mjini.
7 Tazama, ni matusi tu yatokayo mdomoni mwao, maneno yao yanakata kama upanga mkali; tena wanafikiri hakuna anayewasikia.
8 Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wawacheka; unawapuuza hao watu wote wasiokujua.
9 Nitakungoja, ewe uliye nguvu yangu; maana wewe, ee Mungu, u ngome yangu.
10 Mungu wangu utanijia na fadhili zako, utaniwezesha kuwaona maadui zangu wameshindwa.
11 Usiwaue mara moja, watu wangu wasije wakasahau; ila uwayumbishe kwa nguvu yako, uwaporomoshe chini. Ee Bwana, wewe ndiwe ngao yetu!
12 Wao hutenda dhambi kwa yote wasemayo, kwa hiyo na wanaswe katika kiburi chao! Kwa sababu ya laana na uongo wao,
13 uwateketeze kwa hasira yako, uwateketeze wasiwepo tena; ili watu wote wajue kuwa wewe ee Mungu watawala wazawa wa Yakobo hata mpaka miisho ya dunia.
14 Kila jioni maadui hao hurudi wakibweka kama mbwa, na kuzungukazunguka mjini.
15 Hupitapita huko na huko wakitafuta mlo, na wasipotoshelezwa hunguruma.
16 Lakini mimi nitaimba sifa za nguvu yako; nitashangilia asubuhi juu ya fadhili zako; maana wewe umekuwa ngome yangu na kimbilio langu wakati wa taabu.
17 Ewe uliye nguvu yangu, nitakuimbia sifa; ee Mungu, wewe u ngome yangu; Mungu mwenye kunifadhili!

Generic placeholder image