36

Uovu wa binadamu
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu)
1 Dhambi huongea na mtu mwovu, ndani kabisa moyoni mwake; jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake.
2 Mwovu hujipendelea mwenyewe, hufikiri uovu wake hautagunduliwa na kulaaniwa.
3 Kila asemacho ni uovu na uongo; ameacha kutumia hekima na kutenda mema.
4 Alalapo huwaza kutenda maovu, hujiweka katika njia isiyo njema, wala haachani na uovu.

Wema wa Mungu
5 Fadhili zako ee Mwenyezi-Mungu zaenea hata mbinguni; uaminifu wako wafika mawinguni.
6 Uadilifu wako ni kama milima mikubwa, hukumu zako ni kama vilindi vya bahari. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wawalinda wanadamu na wanyama
7 Jinsi gani zilivyo bora fadhili zako! Wanadamu hukimbilia kivulini mwa mabawa yako.
8 Wawashibisha kwa utajiri wa nyumba yako; wawanywesha kutoka mto wa wema wako.
9 Wewe ndiwe asili ya uhai; kwa mwanga wako twaona mwanga.
10 Uendelee kuwafadhili wale wanaokutambua; uzidi kuwa mwema kwa wanyofu wa moyo.
11 Usikubali wenye majivuno wanivamie, wala watu waovu wanikimbize.
12 Kumbe watendao maovu wameanguka; wameangushwa chini, hawawezi kuinuka.

Generic placeholder image