65

Wimbo wa shukrani
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi: Wimbo)
1 Wastahili sifa, ee Mungu, huko Siyoni, watu watakutimizia wewe ahadi zao,
2 maana wewe wajibu sala zetu. Binadamu wote watakujia wewe.
3 Tunapolemewa na makosa yetu, wewe mwenyewe watusamehe.
4 Heri wale unaowachagua na kuwaleta karibu, waishi katika maskani yako. Sisi tutatoshelezwa na mema ya nyumba yako; mema ya hekalu lako takatifu.
5 Kwa matendo yako makuu watuitikia na kutuokoa, ewe Mungu wa wokovu wetu; wewe ndiwe tumaini la viumbe vyote, duniani kote na mbali baharini.
6 Kwa nguvu yako uliisimika milima mahali pake. Wewe una nguvu mno!
7 Watuliza mshindo wa bahari na wa mawimbi yake, wakomesha ghasia za watu.
8 Ulimwengu wote washangazwa na matendo yako. Wasababisha furaha kila mahali, toka mashariki hata magharibi.
9 Wewe waitunza nchi kwa kuinyeshea mvua, waijalia rutuba na kuistawisha; mto wako umejaa maji tele, waifanikisha nchi na kuipatia mavuno. Hivi ndivyo uitengenezavyo nchi:
10 Mashamba wayanyeshea mvua kwa wingi, na kuyalowanisha kwa maji; ardhi wailainisha kwa manyunyu, na kuibariki mimea ichipue.
11 Wautunukia mwaka wote mema yako, kila ulipopitia pamejaa fanaka.
12 Mbuga za majani zimejaa mifugo, milima nayo imejaa furaha.
13 Malisho yamejaa kondoo, mabonde yamefunikwa kwa ngano. Kila kitu kinashangilia kwa furaha.

Generic placeholder image