61

Kuomba ulinzi
(Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Daudi)
1 Ee Mungu, usikie kilio changu, usikilize sala yangu.
2 Ninakulilia kutoka miisho ya dunia, nikiwa nimevunjika moyo. Uniongoze juu kwenye mwamba mkubwa
3 maana wewe ndiwe kimbilio langu, kinga yangu imara dhidi ya adui.
4 Naomba nikae nyumbani mwako milele nipate usalama chini ya mabawa yako.
5 Ee Mungu, umezisikia ahadi zangu, umenijalia sehemu yangu unayowapa wale wakuchao.
6 Umjalie mfalme maisha marefu, miaka yake iwe ya vizazi vingi.
7 Atawale milele mbele yako, ee Mungu; fadhili na uaminifu wako vimlinde.
8 Hivyo nitakuimbia nyimbo za sifa, nikizitekeleza ahadi zangu kila siku.

Generic placeholder image