----------------------------------------
Kipindi cha Noel
Misa hii inasaliwa tarehe 24 Desemba, wakati wa jioni, au kabla au baada ya Vesperi ya Kwanza
ya Noeli.
----------------------------------------
Des 24 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: 2Sam.7:1-5,8-11,16
Ikawa, mfalme Daudi alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo Bwana alipomstarehesha, asiudhiwe na adui
zake waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba
ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote
yaliyomo moyoni mwako; maana Bwana yu pamoja nawe. Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani
kusema, Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae
ndani yake? Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, Bwana wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa
katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli; nami nimekuwa
pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu,
kama jina la wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate
kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam,
kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha
mbele ya adui zako wote. Tena Bwana anakuambia ya kwamba Bwana atakujengea nyumba. Na nyumba yako, na ufalme
wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.89:1-4,27,29
1. Fadhili za Bwana nitaziimba milele;
Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. (K)
(K) Fadhili za Bwana nitaziimba milele.
2. Nimefanya agano na mteule wangu,
Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu.
Wazao wako nitawafanya imara milele,
Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. (K)
3. Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza,
Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.
Wazao wake nao nitawadumisha milele,
Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Ee utokaye Mashariki uliye mng'ao wa mwanga wa milele na jua la haki, njoo uwaangazia wakao
gizani na katika kivuli cha mauti.
Aleluya.
INJILI: Lk.1:67-79
Siku zile, Zakaria, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema, Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,
Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi
wake. Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu; Tuokolewe na adui zetu Na mikononi
mwao wote wanaotuchukia; Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake takatifu; Uapo aliomwapia
Ibrahimu, baba yetu, Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu, Kwa
utakatifu na kwa haki Mbele zake siku zetu zote. Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu, Kwa maana
utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake; Uwajulishe watu wake wokovu, Katika kusamehewa
dhambi zao. Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, Kuwaangaza
wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.
------------
NOVENA YA NOELI
Kama inasaliwa hufuata mara baada ya Injili, na huchukua
sehemu ya sala za waamini
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu zangu, kwa kuwa Mkombozi wetu anakaribia zaidi sasa kuliko wakati ule tulipoanza kuamini, tunahitaji sana
msaada wa Mungu ili maandalizi tunayoyafanya yapate baraka na ulinzi wake:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uilinde mioyo yetu iliyotakaswa tayari, ili isichafuke tena, na uwaamshe ambao bado hawajajipatanisha
nawe, ili wayatumie vema masaa haya machache yaliyosalia.
2. Ujio wa Mwanao utuimarishe tusimame imara katika imani yetu ya kikristo mbele ya adui zetu na wote
wanaotuchukia, ili nao wakuongokee wewe.
3. Uifanikishe sherehe inayokuja, ili tumwabudu Mkombozi wetu pasipo hofu, kwa utakatifu na kwa haki.
4. Uwaangaze wakaao katika giza na uvuli wa mauti na kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.
Ee Baba mwema, tunatambua kwamba mtoto atakayezaliwa ndiye Nabii atokaye juu na Mwenye kutuletea wokovu.
Utujalie sisi sote tuwe makao yake yasiyo na hila yoyote, ili naye akae kwetu siku zote. Anayeishi na kutawala,
daima na milele. Amina.