KITUBIO CHA MTU MMOJA

Generic placeholder image

A: Kupekuwa Dhambi:

1. Pima mwenendo wako mbele ya Mungu.
2. Pima mwenendo wako mbele ya wenzako
3. Kama una ndoa, jipime kama umekaa vizuri katika ndoa yako.
4. Pima matendo yako nafsini mwako mwenyewe.

B: Kuungama Dhambi:

Unapongoja zamu yako ya kuungama usali na kujiweka tayari. Unapoingia katika kiungamio sema hivi:

M: Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu: Amina.

Padri nibariki kwa kuwa nimetenda dhambi.


Padri anamkaribisha anayetaka kuungama kwa maneno kama haya:

P: Bwana awe moyoni mwako, akusaidie kukiri makosa yako, na kuyatubu.

Mwenye kuungama husema:

M: Namwungamia Mungu mwenyezi nawe Padri wangu. Sikuungama tangu....... Niliondolewa dhambi, nikatimiza malipizi. Dhambi zangu ni hizi.......

Taja dhambi ulizokosa na mara ngapi umezitenda. Usiungame ovyo ovyo tu bila kutubu, au kama huna moyo wa kuziacha. Nibure kuungama bila majuto. Ukimaliza sema:

M: Najuta dhambi zangu zote. Ee Yesu unihurumie.
Sikiliza mafundisho ya Padri, na kuyapokea lowa unyenyekevu. Usifanye ubishi. Kumbuka kwamba ndiye Yesu Kristo mwenye kukuondolea na kukutakasa kwa maneno ya Sakramenti anayotamka Padri.

Padri anaweza pia kukuambia usali sala ya kutubu:


SALA YA KUTUBU:
Mungu wangu, nimetubu sana dhambi zangu, kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza, wachukizwa na dhambi. Basi sitaki kukosa tena, nitafanya kitubio, naomba neema yako nipate kurudi. Amina.

Padri anamnyoshea mikono miwili, au mkono wa kuume tu, yule anayeungama, akisema:

P: Mungu, Baba mwenye huruma, aliupatanisha ulimwengu na nafsi yake, kwa kifo na ufufuko wa mwanawe; akushushie Roho Mtakatifu upate kuondolewa dhambi. Yeye mwenyewe akusamehe na kukupa amani kwa huduma ya Kanisa.

Nami nakuondolea dhambi zako kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.

Mwungamaji hujibu:

M: Amina.

P: Bwana amekuondolea dhambi zako. Nenda na amani.

M: Tumshukuru Mungu.

Timiza malipizi uliyopewa:

Unaporudi pahali pako, umshukuru Mungu aliyekuondolea dhambi zako, ukumbuke mashauri aliyokupa Padri, ufanye malipizi yako, na kumwomba Mungu akusaidie usifanye dhambi tena. Malipizi uliyoamriwa ni madogo sana. Kwa hiyo uongeze neno kwa hiari yako. Yawezekana kusali Rozari, kushiriki Misa kila siku ya kazi, kusoma Injili, kuwasaidia wenye shida, kuwashauri wenzako kwenda Kanisani kwa Misa, kuwagawia chakula wenye njaa, kuwatazama wagonjwa, kuwafurahisha wenzako, kuwaamkia watu hisani, na kadhalika. Ukumbuke tena kusudio lako la pekee. Uzoee kurudia kusudio hilo asubuhi na kujiuliza jioni jinsi ulivyolishika.