F

Mordekai anaikumbuka ndoto yake
1 Mordekai akasema, “Mungu ndiye aliyesababisha mambo haya yote.
2 Sasa nakumbuka ndoto niliyoota kuhusu mambo haya, na kila kitu kimefanyika kama nilivyoona ndotoni:
3 Kulikuwa na chemchemi ndogo ambayo ilipanuka ikawa mto; kulikuwa na mwangaza na jua na maji mengi. Mto huo ni Esta, aliyeolewa na mfalme na kufanywa malkia.
4 Yale majoka mawili ni Hamani na mimi.
5 Mataifa ni wale wote waliokusanyika pamoja kuwaangamiza Wayahudi.
6 Taifa langu ni Israeli lililomlilia Mungu, nalo likaokolewa. Bwana aliwaokoa watu wake! Alitukomboa kutoka maovu haya yote na kufanya miujiza na maajabu ambayo kamwe hayajawahi kufanywa katika taifa lolote.
7 Ndio maana yeye aliweka hali mbili tofauti, moja kwa ajili ya Wayahudi, watu wake mwenyewe, na nyingine kwa ajili ya watu wa mataifa mengine.
8 Ndipo ilipofika siku na saa ambayo hali hizi mbili ilibidi ziamuliwe; wakati ukafika wa Mungu kuamua juu ya mataifa mengine.
9 Kwa hiyo Mungu aliwakumbuka watu wake, akawapa haki wanayostahili.
10 Hivyo kila mwaka, nyakati zote zijazo, watu wa Mungu watakusanyika mbele yake siku ya kumi na nne na kumi na tano katika mwezi wa Adari, na kusherehekea kwa furaha, kizazi hadi kizazi.”

Tafsiri ya Kitabu cha Esta Kigiriki
Katika mwaka wa nne wa utawala wa Tolemai na mkewe Kleopatra, mtu fulani aliyeitwa Dositheo aliyedai kuwa ni kuhani Mlawi, alileta barua kuhusu sikukuu ya Purimu. Alikuwa amefuatana na mtoto wake wa kiume aliyeitwa Tolemai, nao wakatangaza kuwa barua hiyo ilikuwa halali na kuwa ilikuwa imefasiriwa na Lisimako, mtoto wa kiume wa Tolemai, mmoja wa wakazi wa mji wa Yerusalemu.

Generic placeholder image