C

Sala ya Mordekai
1 Kisha Mordekai akamwomba Bwana, akikumbuka yale ambayo Bwana alikuwa ameyatenda zamani.
2 Akaomba hivi: “Ee Bwana, Bwana unayetawala ulimwengu wote, na ambaye kwa uwezo wako vitu vyote vipo. Ikiwa ni makusudi yako kuiokoa Israeli, hakuna yeyote awezaye kukupinga.
3 Wewe uliumba mbingu na dunia na mambo ya ajabu yaliyomo duniani.
4 Wewe ni Bwana wa vyote, wala hakuna yeyote awezaye kukupinga, wewe uliye Bwana.
5 Wewe unajua yote. Ee Bwana, unajua kuwa nilikataa kumsujudia Hamani, yule mwendawazimu, si kutokana na kiburi au ujeuri au kujitakia heshima mbele ya watu.
6 Ningaliridhika kujitupa chini, mbele ya Hamani na kubusu nyayo zake kama tendo hilo lingaliiokoa Israeli.
7 Lakini sikutenda hivyo nisije nikamtukuza binadamu badala ya Mungu. Mimi nakataa kumsujudia yeyote isipokuwa wewe Bwana wangu. Na hata hapo si kwa sababu ya majivuno.
8 Sasa, ee Bwana, Mungu na Mfalme, Mungu wa Abrahamu, utuhurumie, utuokoe na adui zetu. Adui zetu wanatutafuta nafasi ili watuangamize. Wanatamani kuwaangamiza watu wako ambao ni mali yako tangu kale.
9 Usiitupe milki ambayo ulijikombolea kutoka utumwani nchini Misri.
10 Ee Bwana, litegee sikio ombi langu. Uuonee huruma urithi wako. Geuza maombolezo yetu kuwa furaha ya sikukuu, nasi tuliimbie sifa jina lako. Usiwaangamize wanaokusifu.”
11 Basi, watu wote wa Israeli wakamlilia Mungu kwa sauti, kwani walijua kwa hakika wanakabiliwa na kifo.

Sala ya Esta
12 Kwa uchungu mwingi, malkia Esta akamgeukia Bwana katika sala.
13 Akayatupilia mbali mavazi ya fahari, akavaa mavazi ya matanga na huzuni. Badala ya kujipaka manukato ya bei kubwakubwa, akajipaka majivu na samadi kichwani. Akafanya kila aliloweza kuufanya mwili wake kuwa mnyonge kabisa. Mwili wake ambao alipenda kuuremba sana, akauacha ufunikwe na nywele zake zisizochanwa.
14 Akamwomba hivi Bwana Mungu wa Israeli: “Ee Bwana wangu, wewe pekee ndiwe mfalme wetu. Nisaidie mimi niliye pweke, na bila yeyote wa kunisaidia, ila wewe tu.
15 Maisha yangu yanakaribia kuisha.
16 Ee Bwana, tangu kuzaliwa kwangu, kwenye kabila na ukoo wangu, nimesimuliwa juu yako kuwa ulichagua taifa la Israeli kati ya mataifa yote kuwa mali yako. Yote uliyowaahidi uliyatimiza.
17 Lakini sasa tumetenda dhambi dhidi yako, nawe umetutia mikononi mwa adui zetu.
18 Umefanya hivyo kwa sababu tuliabudu miungu yao. Lakini wewe ni mwadilifu, Bwana.
19 Hata hivyo, adui zetu hawatosheki ya kuwa tuko kwenye utumwa mkali. Wao wameiapia miungu yao,
20 si tu kuwaangamiza watu wanaokusifu wewe, bali hata na kufutilia mbali sheria yako na kuitokomeza milele madhabahu yako na utukufu wa nyumba yako.
21 Wanakusudia kuufanya ulimwengu wote kuisifu miungu isiyo na maana na kumtukuza mfalme, binadamu afaye.
22 “Ee Bwana, usiiachie uwezo wako hiyo miungu ambayo si kitu wala kuwapa nafasi adui zetu watucheke tunapoangamia. Bali geuza njama zao dhidi yao wenyewe na yule aliyehusika na njama hizo awe wa kwanza kuangamia.
23 Utukumbuke, ee Bwana. Ujijulishe kwetu wakati huu wa taabu, na kunitia moyo mimi, ee Mfalme wa miungu na Bwana wa falme zote.
24 Nijalie ufasaha wa kusema mbele ya yule aliye kama simba na kugeuza moyo wake amchukie huyo mtu aliyepanga njama za kutuangamiza ili aangamie mwenyewe pamoja na wale waliokubaliana naye.
25 Lakini, utuokoe sisi kwa mkono wako. Nisaidie mimi niliye pweke na sina msaidizi yeyote ila wewe tu, ee Bwana.
26 “Ee Bwana, wewe wajua kila kitu. Wewe wajua kuwa nachukia fahari ya waovu, na ni chukizo kwangu kulala na watu hawa wasiotahiriwa, na mtu yeyote asiye Myahudi.
27 Lakini unajua kuwa sina uchaguzi wowote. Naichukia taji ambayo nalazimika kuivaa kama malkia wakati wa shughuli za kifalme. Siivai kamwe wakati mwingine wowote; naichukia kama kitambaa kilichotumika wakati wa hedhi.
28 Mimi mjakazi wako sijawahi kula mezani kwa Hamani, wala sijaheshimu sikukuu ya mfalme na kamwe sijanywa divai yake anayoitoa kuwa tambiko la kinywaji.
29 Sijapata kufurahi tangu siku ile nilipoletwa hapa, isipokuwa furaha yangu ni kukuabudu wewe Bwana Mungu, wa Abrahamu.
30 “Ewe Mungu mwenye nguvu juu ya wote, usikie sauti ya watu wanaokata tamaa, utuokoe makuchani mwa watenda maovu. Uniondolee hofu yangu.”

Generic placeholder image